UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi UWT Kata ya Kivukoni jijini Dar es Salaam katikakati ya wiki hii uliadhimisha Siku ya Wanawake duniani kwa kuendesha Kampeni ya Upimaji Afya kwa wanawake wa jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni ishara ya kuthamini afya ya mwanamke katika maendeleo ya taifa.
Uzinduzi wa kampeni hiyo ulifanyika katika viwanja vya Karimjee, uliwavuta wanawake wengi waliofika kupima afya zao na kukutana na watalaamu mbalimbali wa masuala ya afya, huku mgeni rasmi katika hafla hiyo akiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapunduzi Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu.
Akizungumza kabla ya uzinduzi wa kampeni hiyo Mwenyekiti wa UWT Kata ya Kivukoni, Mariam Kimbisa alisema wameamua kuadhimisha Siku ya Mwanamke duniani kwa upimaji wa afya, kwa kua UWT Kata ya Kivukoni inaamini afya ndiyo mtaji katika shughuli za maendeleo na kueleza kampeni hiyo ni endelevu itakuwa ikifanyika kila mwaka Machi 8.
Mariam amesema umefika wakati sasa kwa wanawake na wasichana kupewa nafasi sawa na wanaume katika maeneo ya kazi, na pia ni wakati sasa kuona kuwa mwanamke si kiumbe dhaifu asiyejiweza, bali kutambua kuwa mwanamke ni nguvu kubwa katika jamii anapopewa nafasi.
“Wanawake ni jeshi kubwa, sisi UWT Kata ya Kivukoni tunayofuraha kubwa ya kumshukuru Mwenyekiti wetu wa chama Mkoa wa Dar es Salaam ndugu Abbas Mtemvu ambaye amekuja kujumuika nasi na kutuunga mkono katika kampeni hii muhimu katika kuadhimisha siku ya mwanamke duniani
“Katika kutambua siku ya wanawake duniani UWT Kata ya Kivukoni tumeamua kuadhimisha siku hii kwa kutoa huduma ya afya bure kwa akina mama. Tunatumia siku hii kuhamasisha wanawake kutambua umuhimu wa afya bora na vile vile upatikanaji wa huduma za fya bora
“Hii inawezekana kwa kila mwanamke kuwa ana afya bora tukiunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wetu mpendwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe Dk Samia Suluhu Hassan katika kuhakikiha wanawake wote nchini wanapata huduma bora ya afya, kwani ukimponya mwanamke umeponya taifa, alisema Mariam.
Machi 8 kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake, ambapo katika siku hii, wanawake wanakutana na kujadiliana kuhusu mafanikio waliyopata katika sekta mbalimbali, changamoto wanazopitia na jinsi ya kukabiliana nazo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es salaam Abbas Mtemvu akimpongeza Mwenyekiti wa UWT Kata ya Kivukoni Mariam Kimbisa kwa niaba ya umoja wa wanawake kata kwa kampeni hiyo ya afya