Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi (kulia) akimsalimia Mwanasheria Mkuu wa Kampuni uya Geita Gold Mining Limited (GGML) David Nzaligo.
NA MWANDISHI WETU
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kuanzisha program zinazolenga kufungua fursa mbalimbali zinazowainua wanawake kielimu, kijamii na kiuchumi.
Pia ameipongeza kampuni hiyo kwa kuendelea kujali wananchi wanaozunguka mgodi huo kupitia mpango wa uwajibika wa kampuni kwa jamii (CSR) pamoja na kutekelezwa matakwa ya sheria madini kiasi cha kuwa mshindi zaidi ya mara mbili katika tuzo za mlipa kodi mkubwa wa sekta ya madini.
Michuzi ametoa kauli hiyo hivi karibuni katika mahoajino maalumu na mwandishi wetu Mjini Geita kuhusu siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8.
Alisema GGML na halmashauri hiyo wamekuwa wakishirikiana vizuri katika program za kuwajengea uwezo wasichana kupitia shule wanazosoma.
Alitolea mfano mwaka jana kwamba walitoa mafunzo maalumu kwa wanafunzi wa Shule ya Wasichana Nyankumbu iliyopo mkoani Geita.
“Mwaka huu tuitafanya kwenye shule nyingine ambapo tutakusanya wasichana wa shule za sekondari na msingi ili kuwahasisha kuona namna gani wanawake tuna nafasi sawa na wanaume katika kutimiza malengo ya taifa zima,” alisema.
Pamoja na ushirikiano huu aliwasihi wadau wa mkoa huo kuwa mfano wa kuigwa kama GGML ambao wamekuwa wadau wazuri kiasi cha kushinda tuzo zaidi ya mbili kila mwaka kwa kuwa mlipa kodi bora.
“Ina maana GGML inaunga mkono serikali kutoa huduma bila kuwa na vikwazo vya kibajeti. Kwa hiyo ushirikiano unahitajika na sisi tulioaminiwa kwa niaba ya serikali tutawapa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha lengo na adhma ya serikali kutatua changamoto za wananchi linafikiwa,” alisema.
Akizungumzia siku ya mwanamke duniani, Michuzi alisema hii ni siku ambayo inamkumbusha kwamba wanawake nao wana uwezo sawa na jinsia nyingine.
“Nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuamini katika jinsia ya kike hususani sisi tulio katika umri mdogo, ukilinganisha na dhana iliyokuwepo hapo zamani kwani kwa umri wetu usingeteuliwa kupewa majukumu makubwa.
“Lakini pia tunashukuru kwa imani yake kwetu imetufanya tujiamini na kujituma kumuaminisha kuwa hakututeua kwa bahati mbaya wala kufanya makosa kwa sababu tuna uwezo, nia na nguvu sawa na wanaume waliokuwa wakiaminiwa hapo zamani.
“Niwasihi viongozi wengine wendelee pia kuamini wasichana na wanawake wenye uwezo katika maeneo wanayowaongoza ili kuwainua na kuwaaminisha kuwa wanaweza kufanya makubwa zaidi ya sisi tulioaminiwa sasa,” alisema.
Aidha, aliwashauri mabinti wadogo na wanawake wenzake kwamba wajiamini kuwa wanaweza, waamini kipawa Mungu alichowapa na wasijidharau hata wanapopitia misukosuko ya kurudishwa nyuma, waseme ili kumsaidia mwingine aliyekwama ainuke na kusaidiwa kwa sababu taasisi zipo nyingi, kuanzia serikali na taasisi binafsi.
Alitoa wito kwa wanawake kutoa vipawa walivyonavyo wasivifiche, kwa sababu serikali ipo kuwaunga mkono ikiwa ni pamoja na GGML kuhakikisha mwanamke harudishwi nyuma ili waende kwenye usawa ambao wanaupigania kwa sasa.
GGML imekuwa ikitekeleza program mbalimbali za kuwainua wanawake ikiwamo program ya Female Future Tanzania Programme (FFT) ambayo inaratibiwa na Chama cha Waajiriwa Tanzania (ATE) kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake kushika nyadhifa za juu.
Pia kampuni hiyo ambayo hutoa kipaumbele cha ajira kwa wanawake, inatekeleza program ya masomo ya shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara (MBA) pamoja na program nyingine za mafunzo ndani ya kampuni kwa lengo la kuwainua wanawake kushika nafasi za juu za uongozi.