Featured Kitaifa

POLISI WATETA NA MAKUNDI MBALIMBALI KUJADILI NAMNA YA KUMALIZA MAUAJI MKOANI KAGERA

Written by mzalendoeditor

 

Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi.

Kamishna wa Polisi Jamii Nchini, CP Faustine Shilogile amewataka Wakaguzi wa Kata waliopelekwa katika Kata zote hapa nchini kufanya kila jitihada za kushirikiana na Watendaji wa Kata, Vijiji na viongozi wa serikali ngazi za chini kuzuia uhalifu na sio kupambana na uhalifu.

Kamishna Shilogile amesema hayo leo alipokua katika mkutano na makundi mbalimbali wakiwemo wazee wa kimila, viongozi wa dini, watendaji wa Kata, wazee mashuhuri na Kamati ya Amani Wilaya ya Misenyi, Mkoa wa kagera wakati wa ziara yake ya kuhakikisha wanamaliza tatizo la mauaji yanayoendelea mkoani humo.

CP Shilogile amesema ni wakati sasa wa viongozi hao kushirikiana kwa pamoja katika kukemea na kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya uhalifu katika maeneo yao.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara katika soko la Bunazi Wilayani Misenyi Mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mstaafu wa Polisi, SACP Engelbert Kiondo amesema pamoja na Polisi Kata kupelekwa kwenye Kata kuzuia uhalifu lakini pia watakua msaada kwa vijana walioathirika na dawa za kulevya akitolea mfano bangi na pombe.

SACP Kiondo amebainisha kuwa kwasababu vijana hao wameshakua waathirika wa dawa hizo hivyo kupitia Polisi Kata hao watatumia nafasi zao kutafuta wataalamu kwaajili ya kuwaelimisha ili kuwaondoa katika utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na ulevi uliokithiri.

Kamishna wa Polisi Jamii yupo Mkoani Kagera akizungumza na makundi mbalimbali kutafuta muarubaini wa kumaliza tatizo la mauaji yanayoendelea Mkoani humo kwa sababu za wivu wa mapenzi, migogoro ya ardhi na Imani za kishirikina. 

About the author

mzalendoeditor