Featured Kitaifa

GGML YASHINDA TUZO YA KIMATAIFA YA USALAMA KWA MWAKA WA 4 MFULULIZO

Written by mzalendoeditor

Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo wa GGML, Dkt Kiva Mvungi (wa pili kulia) pamoja na watendaji wa idara ya afya na usalama kutoka Geita Gold Mining Limited wakifurahia ushindi wa nne mfululizo katika tuzo ya kimataifa ya usalama mahala pa kazi. Kampuni hiyo imeiongoza Tanzania imezipiku nchi za Australia, Ghana na Afrika Kusini.

NA MWANDISHI WETU

MISINGI imara ya udhibiti wa hali ya usalama katika utendaji kazi ndani na nje ya Mgodi wa Geita Gold Mining Limited. (GGML), imeendelea kuifanya kampuni hiyo kuandika historia duniani baada ya kushinda  kwa mara ya nne mfululizo tuzo ya kimataifa ya usalama mahala pa kazi (Global Safety Award).

Katika tuzo hiyo inayotolewa na kundi la makampuni ya AngloGold Ashanti (AGA), GGML imeshinda mwaka 2019, 2020, 2021 na wiki hii imeshinda tuzo hiyo kwa mwaka 2022.

Akizungumzia ushindi huo katika mahojiano maalumu na Mwandishi wetu mkoani Geita, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo wa GGML, Dkt Kiva Mvungi alisema tuzo hiyo inamaanisha kuwa AGA imeitambua GGML kama kampuni kinara inayofanya vizuri katika masuala ya usalama duniani.

AGA ambayo imeorodheshwa katika masoko ya hisa ya Johannesburg, New York, Australia na Ghana inamiliki migodi katika nchi za Australia, Columbia, Argentina, Brazil, Ghana na Tanzania. Katika nchi zote hizo,GGML au Watanzania kwa ujumla ndio vinara wa kuzingatia masuala ya usalama mahala pa kazi.

Dkt Kiva Mvungi alisema mafanikio hayo hayakuja kirahisi kwani GGML imefanikiwa kuimarisha ushirikiano wa wafanyakazi ambao wamekuwa wakiuonesha katika kujali afya zao pamoja na kujali usalama kazini.

Alisema kitu ambacho wamefanya tofauti na wenzao ni kwamba walibadilisha mfumo wa mawasiliano ya kiusalama, badala ya kutoka kwa viongozi kwenda kwa wafanyakazi, waliweka utaratibu kwamba mfumo huo wa mawasiliano utoke kwa wafanyakazi kuja kwa viongozi.

“Kwa hiyo tunapofanyakazi, wafanyakazi hutuambia hii ni salama au sio salama au angetaka ifanyike vipi, kwa hiyo sisi huongeza tu masuala mengine ya kiuongozi kuhakikisha suala linafanikiwa,” alisema. 

Alisema tangu wameanza kutumia mfumo huo wa kuwasikiliza zaidi wafanyakazi, mafanikio yamekuwa makubwa katika utendaji kazi. Anatolea mfano kuwa zaidi ya miaka 10 hawajapoteza maisha ya mfanyakazi yeyote kazini, lakini zaidi ya miaka mitano hakuna mfanyakazi aliyeumia kiasi cha kushindwa kuingia kazini. Pia wamekaa zaidi ya miaka minne bila ya kuwa na mtu aliyeumia kazini.

Aidha, alimpongeza kila mtu aliyeshiriki kuhakikisha mfanyakazi au mkandarasi anapokuja kazini anafanya kazi kwa usalama na anaondoka nyumbani kwa usalama.

Aidha, akizungumza ushindi huo wa tuzo nne mfululizo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong aliipongeza timu nzima ya idara ya afya, usalama na mazingira pamoja na wafanyakazi wote wa GGML kwa kudumisha usalama wao ndani na nje ya kampuni.

Mbali na tuzo hiyo ya kimataifa ya usalama, anasema GGML pia ilipata tuzo ya utendaji bora wa jumla.

“Hakika tuzo hii inaonesha namna tunavyofanya vizuri na kuthaminiwa. Juhudi zenu zinatambuliwa vyema na kampuni nzima. Kama tunavyojua sote bado tuna changamoto nyingi za kufanyia kazi kama timu lakini nina uhakika tunaweza kufanya kazi pamoja na kutimiza yote tuliyojiwekea Kongole kwenu wote.,” alisema Mkurugenzi huyo.

Mmoja wa wafanyakazi wa idara hiyo ya usalama, afya na mazingira ndani ya GGML, Dkt. Subira Joseph ambaye amefanya kazi ndani ya kampuni hiyo kwa zaidi ya miaka 10 kama daktari kwenye kituo cha afya cha GGML pamoja na Josephine Kimambo ambaye ni mhandisi wa mazingira, walisema ushindi mfululizo wa tuzo hiyo, umewafanya waone wanafanya kazi kwenye mazingira salama.

“Mazingira ya kazi yasingekuwa salama hata tuzo hii tusingeipata. Lakini pia imenifanya nione idara yetu ya usalama, afya na mazingira kazini inafanya kazi vizuri na watu,” alisema Josephine.

About the author

mzalendoeditor