Featured Kitaifa

WRRB YAKUSANYA KILO BILIONI 2.3 ZA MAZAO NCHINI

Written by mzalendoeditor

MKURUGENZI Mtendaji wa Bodi  ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) Asangye Bangu akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ,wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za bodi hiyo leo Februari 15,2023,jijini Dodoma.

Na. Alex Sonna-DODOMA

IMEELEZWA  tangu kuanzishwa kwa mfumo wa stakabadhi za Ghala mwaka 2007, zaidi ya kilo bilioni 2.3 za mazao mbalimbali zimekusanywa katika maeneo mbalimbali nchini.  

Kauli hiyo imetolewa leo Februari 15,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi  ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) Asangye Bangu,wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Bodi hiyo kwa waandishi wa habari.
“Toka kuanza kwa mfumo huu tumefanikiwa kukusanya zaidi ya kilo bilioni 2.3 za mazao 11 yaliyomo kwenye mfumo mazao hayo ni alizeti, choroko, dengu, kahawa, kakao, korosho, mahindi mbaazi,mpunga,soya pamoja na ufuta”amesema Bw.Bangu

Aidha amesema kuwa  mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa Stakabadhi za Ghala ni pamoja na ongezeko bei la  za mazao, mapato ya mkulima na mapato ya serikali kwa wastani wa asilimia 200 kutokana na urasimishaji.

“Mafanikio mengine ni ongezeko la uzalishaji wa mazao kwa wastani wa asilimia 12 kwa mwaka, mfumo huu pia ni kichocheo cha ubora wa mazao yanayofikishwa sokoni, upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao yanayopita kwenye mfumo wa Stakabadhi za Ghala, ongezeko la mapato ya
uhakika kwa serikali kuu na serikali za mitaa, kukuza huduma za fedha vijijini, kufanikisha uanzishaji wa soko la bidhaa Tanzania”ameeleza

Amesema amesema kuwa ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknojia Bodi imekuwa ikishirikiana kwa karibu na kuhamasisha bodi ya TEHAMA kukamilisha mifumo mipya na kuhamishia huduma za Bodi hiyo kwenda kidijitali.
Aidha, Bodi imeendalea juhudi za kuboresha Mfumo uliokuwepo wa kizamani wa Usimamizi wa ghala, ambapo kushirikiana na Bodi ya TEHAMA inakuja na Mfumo mpya wenye kuweza kurahisisha kazi za
maandalizi ya taarifa, utoaji stakabadhi na udhibiti wa matukio ghalani hivyo kupunguza muda wa michakato na kuongeza ufanisi na usalama wa mzigo.
“Majaribio ya Mfumo wa Maombi ya Leseni Mtandaoni yamefanyika na mapendekezo ya maboresho yamepelekwa kwa programmers kwa ajili ya kufanyiwa kazi,”amesema Bangu

Hata hivyo Bw.Bangu ametoa  wito kwa madalali kuacha tabia ya kuwarubuni wakulima na badala yake kuwaacha waingie kwenye mfumo wa Stakabadhi ghalani ili kuuza mazao yao kulingana na bei iliyopo sokoni.

“Natoa wito kwa madalali waache kuwarubuni wakulima wawaache wajiunge katika Mfumo wa Stakabadhi ghalani ili waweze kuuza mazao yao kwa bei ya ushindani iliyopo sokoni kwa kuendelea kuuza mazao shambani inaendelea kuwadidimiza wakulima kwa sababu madalali wengi wananunua mazao kwa bei ya chini tofauti kabisa na bei iliyopo kwenye mfumo,”amesema Bangu

About the author

mzalendoeditor