Featured Kitaifa

SHULE YA SEKONDARI LUKUNDO YAPONGEZW KWA KUFANYA VIZURI KIDATO CHA NNE

Written by mzalendoeditor

AFISA Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu ameipongeza Shule ya Sekondari Lukundo kwa kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne na kufuta daraja sifuri.

Mwalimu Rweyemamu alitoa pongezi hizo alipofanya ziara maalum katika Shule ya Sekondari Lukundo kwa ajili ya kuwapongeza walimu wa shule hiyo na kuwapatia zawadi.

Mwalimu Rweyemamu alisema “nilifurahi sana baada ya kuona matokeo yenu ya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne mwaka 2022 Shule ya Sekondari Lukundo. Nilifurahi sana kuona hamna daraja sifuri hata moja, nilifurahi sana kuona ‘division’ I zilivyo nyingi, ‘division’ II zilivyo nyingi, ‘division’ III zilivyo nyingi. Asanteni sana.

Afisa elimu huyo aliitaja Shule ya Sekondari Lukundo kuwa ni mfano mzuri kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Mmethibitisha kwamba tunapoweka mikakati, tukashikamana tunatoka kwa mafanikio makubwa. Kwa hiyo, hakuna shule yoyote itakayosimama na kusema hatuwezi. Atakayesema hatuwezi nitamwambia nenda Shule ya Sekondari Lukundo ukajifunze” alisema Mwalimu Rweyemamu.

Mwalimu Rweyemamu aliitaka Shule ya Sekondari Lukundo kujipanga kufuta daraja la IV katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne mwaka 2023. “Kama mmeweza kuondoa ziro mwaka 2022, inawezekana kabisa hata daraja la IV mkaliondoa katika matokeo ya mwaka 2023. Ninajua mnamipango mizuri na mikakati mizuri. Nataka kuwa natamba kuwa ninayo Shule ya Sekondari Lukundo inayofanya vizuri” alisisitiza Mwalimu Rweyemamu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Lukundo, Mwalimu Asafu Makonda alisema kuwa shule yake imefanikiwa kuondoa daraja sifuri kutokana na mshikamano uliopo. “Shule ya Sekondari Lukundo imeondoa daraja sifuri hapa Dodoma, Afisa Elimu Sekondari Jiji la Dodoma nikukumbushe tu kuwa hizi ni juhudi na mipango yako wewe mwenyewe. Utakumbuka baada ya matokeo ya moko mwaka 2022, ulikuja na program ya tokomeza ziro. Tuliona dhamira yako ya kufuta ziro na walimu wakatambua wakasema ngoja tupambane kwa mama huyu ambaye ameonesha upendo mkubwa” alisema Mwalimu Makonda.

Ikumbukwe kuwa shule ya sekondari Lukundo imefanikiwa kufuta daraja sifuri katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne mwaka 2022, mwaka 2021 shule hiyo ilipata daraja sifuri tatu. Matokeo jumla yam waka 2022 daraja I (20), daraja II (47), daraja III (43) na daraja IV (116).

About the author

mzalendoeditor