Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS AZINDUA WIKI YA SHERIA DODOMA

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibarahim Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdallah, Viongozi na Watumishi mbalimbali wa Mahakama pamoja na Viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dodoma wakati akiongoza Matembezi ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria yalioanzia katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Haki (IJC) na kumalizika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square) leo tarehe 22 Januari 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiongoza Viongozi na Watumishi mbalimbali wa Mahakama na Mkoa wa Dodoma katika kuimba wimbo wa Taifa mara baada ya kumaliza  Matembezi ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria yalioanzia katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Haki (IJC) na kumalizika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square) leo tarehe 22 Januari 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na Viongozi na Watumishi mbalimbali wa Mahakama pamoja na Viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dodoma mara baada ya Matembezi ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria yalioanzia katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Haki (IJC) na kumalizika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square) leo tarehe 22 Januari 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibarahim Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdallah, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dkt. Eliezer Feleshi,Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel,Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani na Viongozi mbalimbali wa Mahakama mara baada ya Matembezi ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria yalioanzia katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Haki (IJC) na kumalizika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square) leo tarehe 22 Januari 2023.

****************************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mahakama na mfumo wa utoaji haki kwa ujumla kuongeza juhudi katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo suala la Rushwa katika vyombo vya utoaji haki pamoja na suala la upelelezi kuchukua muda mrefu.

Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya Matembezi ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria yaliofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Nyerere Square) Jijini Dodoma leo tarehe 22 Januari 2023.

Amesema yamekuwepo malalamiko katika maeneo ya minada ya mifugo inayokamatwa kwenye hifadhi kuzuiwa au wahusika kutozwa faini ndogo, fedha za kigeni zilizokamatwa mipakani kupotea mikononi mwa mahakama na hukumu kupindishwa ili kumpa ushindi mwenye fedha.

Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kushughulikiwa kwa malalamiko ya gharama kubwa za uendeshaji wa kesi na kulipia gharama za mawakili, hukumu kuandikwa kwa lugha ya kiingereza, watuhumiwa kukaa mahabusu muda mrefu kusubiri uchunguzi kukamilika pamoja na ukosefu wa elimu ya sheria kwa umma. 

Amewaasa wahusika katika mfumo wa utoaji wa haki kuendelea kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha huduma mbadala ya usuluhishi inapatikana na kufikika kwa urahisi.

Katika nyingine Makamu wa Raais ametoa wito kwa Mahakama kushirikiana vema na wadau katika kuimarisha utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi ili kuweza kufikia malengo yake kirahisi.

Amesema mawakili wa kujitegemea wanapaswa kujielekeza  katika kutoa elimu na ushauri sahihi kwa wateja wao kuhusu namna bora ya kutatua migogoro ikiwa ni pamoja na kutumia njia mbadala ya usuluhishi badala ya kuendelea na kesi mahakamani ambako watalipwa gharama kubwa zaidi za kuwatetea.

Makamu wa Rais ameziasa asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kutoa elimu kwa umma, misaada kwa wananchi na kujenga uelewa kuhusu haki za msingi za kiraia na umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa viongozi wa dini na viongozi wa mila kote nchini kuisadia Mahakama kuzungumza na wananchi kuhusu umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.

Dkt. Mpango ameagiza kuangaliwa upya ufanyaji kazi wa mabaraza ya ardhi nchini kutokana na kuongezeka kwa migogoro ya ardhi inayokosa usuluhishi wa mapema.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu imeendelea kuhakikisha Mahakama inakuwa na miundombinu bora, watendaji wa kutosha, pamoja na mazingira wezeshi ya kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo kuhakikisha Mahakama inapata fedha za matumizi ya kawaida, fedha za maendeleo za ndani na pia kukopa mikopo ya masharti nafuu ili kutekeleza miradi ya maboresho ya Mahakama ikiwemo ujenzi wa majengo ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (6) (Integrated Justice Centres), Mahakama za Wilaya (25), Mahakama ya Hakimu Mkazi (1) na Mahakama za Mwanzo (6).

Vilevile amesema ili kuongeza ufanisi na kukidhi mahitaji, Mheshimiwa Rais ameshateua jumla ya Majaji 52 (Mahakama ya Rufani 9 na Mahakama Kuu 43) na kuagiza Wizara ya Mawasiliano, TTCL pamoja na eGA kuhakikisha kuwa Mahakama inapatiwa “Bandwidth” ya kutosha ili kuendesha shughuli zake kwa kutumia Tehama.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa wito kwa wananchi wanaohitaji kudai haki zao kuhakikisha wanafahamu kwanza haki hizo kwa kusoma na kutafuta elimu itakayowezesha kufahamu sheria na taratibu zinazoongoza haki inayotafutwa.

Amesema Wiki ya sheria itatumika katika kutoa elimu na kuwakumbusha wananchi namna ya kupata haki zao kwa njia sahihi na rahisi.

Amesema wiki hiyo pia itatumika kuonesha namna mahakama inavyotumia teknolojia katika kufanya shughuli zake. Prof Juma ameongeza kwamba kwa matumizi ya Tehama, haki inayotolewa mahakamani itakua shidani na haki bora na iliyowazi kwa wananchi na wale watakaofika mahakamani.

Wiki ya Sheria imeanza rasmi leo tarehe 22 Januari 2023 na inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 1 Februari 2023.

About the author

mzalendoeditor