Featured Kitaifa

WAZIRI MKENDA AZINDUA BODI YA TCU JIJINI DODOMA

Written by mzalendoeditor

 

WAZIRI  wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda ,akizungumza wakati akizindua bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) hafla iliyofanyika leo Januari 19,2023 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael ,akizungumza wakati wa uzinduzi wa  bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) hafla iliyofanyika leo Januari 19,2023 jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof.Penina Mlama,akitoa taarifa  wakati wa uzinduzi wa  bodi ya Tume hiyo  hafla iliyofanyika leo Januari 19,2023 jijini Dodoma.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof.Charles Kihampa,akizungumza wakati wa uzinduzi wa  bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) hafla iliyofanyika leo Januari 19,2023 jijini Dodoma.

Sehemu ya Wajumbe wa Bodi wakisikiliza hotuba ya Waziri   wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda (hayupo pichani) wakati akizindua bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) hafla iliyofanyika leo Januari 19,2023 jijini Dodoma.

WAZIRI  wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda ,akikabidhi vitendea kazi kwa baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) mara baada ya kuzindua bodi ya Tume hiyo katika hafla iliyofanyika leo Januari 19,2023 jijini Dodoma.

WAZIRI  wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzindua  bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) hafla iliyofanyika leo Januari 19,2023 jijini Dodoma.

………………………………………

Na Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameitaka Bodi Mpya ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kuhakikisha inatoa taarifa zilizo sahihi ili kuwezesha ongezeko la vyuo vikuu vya umma na binafsi ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la wanafunzi wanaomaliza elimu ya sekondari na kufaulu kujiunga na elimu ya juu.

Hayo ameyasema leo Januari 19,2023 jijini Dodoma wakati akizindua bodi ya tume hiyo ambapo amesema kuwa bodi hiyo ina jukumu la kuhakikisha inawawezesha na kuwasaida wale wanaohitaji kusajili na kufungua vyuo ili kuhakikisha ongezeko litakalokidhi mahitaji ya wanafunzi wanaotakiwa kudahiliwa katika elimu ya juu.

Pia. Prof. Mkenda ameitaka bodi hiyo kuhakikisha inawawezesha watanzania wengi Kwenda kusoma nje ya nchi kwa kuvihakiki vyuo vinavyotoa elimu nje ya nchi hasa vile vinavyotoa mafunzo ya sayansi na kutoa taarifa sahihi kwa wazazi ama wanafunzi wanaohitaji Kwenda kusoma nje.

“Tunahitaji wanafunzi wengi wapate nafasi ya Kwenda kusoma nje ya nchi, hivi karibuni nimekuwa na mkutano na watanzania waishio nje ya nchi lengo likiwa kuwatumia wao kufungua fursa zaidi za watatanzania Kwenda kusoma nje, tunataka tupate wataalam wengi wenye ujuzi wa kutosha kutoka nje” amesema Prof.Mkenda

Aidha Waziri Mkenda  ameitaka  TCU kuendeleza ubora wa elimu katika ngazi ya vyuo vikuu ili kuleta chachu ya ubora wa elimu katika ngazi ya shule za msingi na sekondari.

“Tunalalamika elimu ya msingi na sekondari ni ya ovyo lakini tukumbuke hawa wanaohitimu kutoka katika ngazi za vyuo vikuu ndio wanaokuja kufundisha huku chini, hivyo ni mzunguko, tukiboresha elimu ya vyuo vikuu tutatoa walimu wenye umahiri watakaoleta chachu ya ubora wa elimu katika ngazi ya huku chini” amesisitiza Prof.Mkenda

Hata hivyo Prof.Mkenda amesema kuwa ili kuhakikisha serikali inaimarisha ubora wa elimu ni lazima PhD za kusoma darasani ziwe zinakaguliwa kuona kama waliopewa wanastahili na hili linaweza kufanywa kwa kuhakiki dissertation zao kama ni halisi ama wamecopy pamoja na kufanya presentation za wazi za dissertation hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof.Penina Mlama, amesema kuwa sekta ya elimu ya juu inakuwa kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya vyuo vikuu pamoja na kupanuka kwa mitaala ya kitaaluma inayotolewa.

”Ongezeko hili la vyuo vikuu na udahili katika vyuo hivi unachochewa na fursa zilizofunguliwa na sera bora ya nchi ya kutoa elimu bila malipo katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari.”amesema Prof.Mlama

Hata hivyo Prof.Mlama amesema kuwa bodi inatambua umuhimu wa sekta ya elimu ya juu katika kuleta maendeleo ya nchi kutokana na dhima yake ya kufinyanga na kutoa wataaalam kwa ajili ya sekta zote.

“Tunatambua kuwa sekta ya elimu ya juu  ndio tegemeo kuu la serikali yetu katika kujenga na kuongeza maarifa, ujuzi, na  taaluma kupitia utafiti na uvumbuzi, hivyo tutafanya kazi kwa weledi na kuboresha sekta hii ili kuweza kufikia malengo na matarajio ya serikali” amesema

About the author

mzalendoeditor