Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS AZITAKA MAMLAKA ZA MAJI NA AWADAU KUONGEZA WELEDI USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA MAJI

Written by mzalendoeditor

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt.Philip Mpango akihutubia Viongozi na Wananchi mbalimbali waliojitokeza
katika hafla ya uwekaji Jiwe la Msingi Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria
utakaohudumia Tinde na Shelui leo tarehe 19 Januari 2023 mkoani
Shinyanga.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt.Philip Mpango akisalimiana na Waziri wa Maji Jumaa Aweso mara baada
ya kuwasili Tinde mkoani Shinyanga kwaajili Uwekaji Jiwe la Msingi Mradi wa
Maji wa Ziwa Victoria utakaohudumia Tinde na Shelui unaogharimu shilingi
bilioni 24.4 leo tarehe 19 Januari 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt.Philip Mpango akiwa na Waziri wa Maji Jumaa Aweso, Kaimu Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yahaya Nawanda akivuta kitambaa kuashiria kuweka
Jiwe la Msingi Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria utakaohudumia Tinde na Shelui
unaogharimu shilingi bilioni 24.4 leo tarehe 19 Januari 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt.Philip Mpango akimwagilia mti aina ya Mzeituni (Olive Tree) mara baada
ya kupanda mti huo wakati wa Hafla ya Uwekaji Jiwe la Msingi Mradi wa Maji
wa Ziwa Victoria utakaohudumia Tinde na Shelui unaogharimu shilingi bilioni
24.4 leo tarehe 19 Januari 2023 mkoani Shinyanga.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Dkt.Philip Mpango amezitaka Mamlaka za Maji pamoja na wadau wengine wa
sekta hiyo kuongeza weledi katika usimamizi wa rasilimali za maji kwa
kujenga miundombinu mingi zaidi ya kutunza maji na kuvuna maji ya mvua ili
kukabiliana na changamoto za maji ambazo hujitokeza.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji
wa Ziwa Victoria utakaohudumia Tinde na Shelui unaogharimu shilingi
bilioni 24.4, hafla iliofanyika eneo la Tinde mkoani Shinyanga leo tarehe 19
Januari 2023.

Amewataka kuongeza ufanisi katika matumizi ya maji, hususan
kwenye kilimo pamoja na kuwaagiza kutunza vyanzo vya maji ikiwemo chanzo
cha Ziwa Victoria kilichopo Ihelele Wilayani Misungwi, ambacho ni tegemeo
kwa upatikanaji wa huduma za maji katika Miji ya Wilaya za Misungwi,
Kahama, Shinyanga, Tabora, Kahama, Nzega, Igunga, Shelui na Tinde.

Aidha Dkt. Mpango amesema dhamira ya Serikali ni kuona mradi huo unatoa
maji na kuwa endelevu kwa wananchi kama ilivyokusudiwa na pia juhudi za
kupeleka maji katika maeneo yaliyopo karibu na mradi huo zinaendelea ikiwa
ni pamoja na kuhakikisha maeneo yote yanapata majisafi na salama na
yanatosheleza mahitaji.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kutoa kipaumbele cha
juu kugharamia miradi ya maji ili itoe huduma endelevu ya majisafi na salama
pamoja na elimu ya usafi wa mazingira kwa wananchi wote. Amesema Sekta
hiyo ni miongoni mwa Sekta za kipaumbele katika Mkakati wa kukuza Uchumi
wa Viwanda na kupambana na umaskini nchini.

Amesema kuboresha huduma
ya maji kutapunguza muda wa kutafuta na kuchota maji ili kuwawezesha
Wananchi kufanya kazi nyingine za maendeleo,kuongezeka kwa muda wa
Wanafunzi kuhudhuria masomo, kuimarisha afya za Wananchi na kuepusha
magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.

Halikadhalika Makamu wa Rais amekemea tabia ya wizi wa maji inayofanywa
na baadhi ya watu nchini wakiwemo wawekezaji wakubwa.

Amezitaka
mamlaka kuacha kutoza faini ndogo kwa wanaokutwa na hatia za wizi wa
maji. Aidha amevitaka vyombo vyote husika kufuatilia na kuwachukulia hatua
wezi wote pamoja na wale wanaochepusha maji kutoka kwenye mito bila
vibali halali na wengine kuharibu vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema Wizara hiyo
inatekeleza miradi ya maji ya kimkakati katika mkoa wa Shinyanga
inayogharimu shilingi bilioni 35 itakayosaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa
mkoa huo kuondokana na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama.

Aweso amesema pamoja na wananchi wa kata ya Tinde kunufaika na mradi
huo pia vijiji 22 vya Jirani vitaweza kufikiwa na mradi utakaowasaidia
wananchi kupata maji safi na salama.

Ameongeza kwamba Wizara hiyo
itaendelea kufuatilia na kusimamia kwa makini utekelezwaji wa miradi ya maji
ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kutoka huduma kwa wananchi katika
kufikia adhma ya kufikisha maji kwa asilimia 95 maeneo ya mijini na asilimia
85 maeneo ya vijijini ifikapo mwaka 2025.

Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amehitimisha ziara yake ya
kikazi mkoani Shinyanga.

About the author

mzalendoeditor