Featured Kitaifa

UBALOZI WA MAREKANI KUENDELEZA MASHIRIKIANO NA CHUO CHA MIPANGO DODOMA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

BALOZI wa Marekani nchini Tanzania, Michael Anthony Battle amesema Serikali yake itaendelea kuimarisha uhusiano wa kikazi na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) ili kuchochea kasi na juhudi ya Serikali ya Tanzania katika kutokomeza umaskini.

Ameeleza kufurahishwa na namna ya kitaalamu na kizalendo ambayo chuo hicho kimekuwa kikitekeleza programu mbalimbali za mafunzo ya ujasiriamali na ubunifu zinazoanzishwa na kufadhiliwa na Ubalozi wa Marekani chuoni hapo kwa lengo la kuwakomboa vijana kiuchumi.

Balozi Battle ameyasema hayo alipofanya ziara maalum katika chuo hicho mwishoni mwa wiki kwa lengo la kujionea namna ambayo chuo hicho kinaendelea kuwafundisha vijana juzi mbalimbali za kibiashara na kibunifu.

“Marekani na Tanzania tumekuwa na ushirikiano kwa miaka mingi sasa, na katika nyanja mbali, ikiwemo elimu,” alisema.

Kwa takribani miaka saba sasa, Ubalozi wa Marekani na chuo cha Mipango wakuwa wakishirikiana katika kutekeza programu mbalimbali za mafunzo zinazolenga kuwainua vijana kiuchumi.

“Nilfurahishwa sana kwa namna ambavyo mlisimama kitaalamu katika utekelezaji wa mradi wa ‘Academy For Women In Entrepreneurship (AWE), mradi uliyofadhiliwa na Ubalozi na ambao uliweza kupata matokea chanya katika kuwawezesha vijana wa kike,” alisema.

Kwa upande wake, Chad Morris, Afisa wa Masuala ya Utamaduni, Sehemu ya Masuala ya Umma katika Ubalozi wa Marekani alieleza kuwa wana furaha sana kufanya kazi na IRDP.

“Sisi katika Ubalozi tunajivunia sana kwa uhusiano ambao tumejenga na IRDP kwa miaka saba iliyopita,”
“IRDP ilikaribisha na kuutekeleza kitaalamu mradi wetu wa ujasiriamali kwa wanawake,” alisema.

Morris aliongeza kuwa Ubalozi wa Marekani unatafuta njia zaidi za kuendeleza na kutekeleza programu muhimu zaidi katika chuo hicho cha serikali, hasa programu zinazolenga kuwawezesha vijana .

Kwa upande wake, Mkuu wa chuo cha Mipango, Profesa Hozen Mayaya alisema ziara ya Balozi Battle ni ishara njema ya mwendelezo wa mashirikiano baina ya pande hizo mbili.
“Uhusiano wetu wa kikazi na Ubalozi wa Marekani umedumu kwa miaka saba sasa na kupitia ushirikiano huu wa muda mrefu tumeona na kupata mafanikio mengi,” alisema.

Ameitaja baadhi ya miradi ambayo chuo imefanikiwa kuutekeleza kwa ushirikiano na Ubalozi wa Marekani kuwa ni pamoja na mradi wa ‘Academy for Women in Entrepreneurship (AWE), pamoja na Mipango Entrepreneurship and Innovation (MEI) ambayo yote imejikita katika kuwawezesha vijana wa Kitanzania.
Kwa upande wake, Profesa Provident Dimoso, Naibu Mkuu Taaluma katika chuo cha Mipango, amesema kupitia uhusiano huo na Ubalozi wa Marekani, chuo kimefanikiwa kujenga mashirikiano mazuri na vyuo vikuu mbalimbali vikubwa nchini Marekani.

“Kupitia mashirikiano hayo tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kujifunza mambo mengi kutoka kwa wenzetu, na hivyo kujikuta tunatoa mafunzo katika viwango vya juu sana na vya kisasa zaidi ya vyuo vingi hapa nchini,” alisema.

Kitokana na hatua hiyo, Profesa Dimoso ameeleza kuwa chuo hicho kimekuwa kikipokea ongezeko kubwa sana la wanafunzi kila mwaka.

About the author

mzalendo