Featured Kitaifa

SERIKALI KUZICHUKULIA HATUA SHULE ZINAZOFUNDISHA WANAFUNZI VITENDO VISIVYO NA MAADILI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ,akizungumza na  waandishi wa habari leo Januari 17,2023 wakati akitoa taarifa  kuhusu wanafunzi kufundishwa vitendo visivyo na maadili katika baadhi ya shule kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

…………………………

Na Alex Sonna-DODOMA

SIKU moja baada ya kuripotiwa kwa uwepo wa vitendo vya watoto kufundishwa kulawitiana katika baadhi ya shule nchini, Serikali imemtuma Kamishna wa Elimu,Mkurugenzi wa Udhibiti ubora wa Elimu na Mwanasheria wa Wizara ya Elimu kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 17,2023 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu  wanafunzi kufundishwa vitendo visivyo na maadili katika baadhi ya shule kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Waziri Mkenda amesema kuwa Timu iliyoenda italeta taarifa kamili na  wapo  tayari kuchukua hatua stahiki kudhibiti mambo hayo.

“Tumeshitushwa sana na taarifa hizo,tumeamua kumpeleka Kamishna wa Elimu mwenyewe siyo mwakilishi wake,Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Elimu mwenyewe siyo mwakilishi wake pamoja na mwanasheria wa wizara waende haraka sasahivi wanapitia hizo shule zilizotajwa kujaribu kupata ‘Fact’ ukweli wote ”alisema Prof. Mkenda

Pia, amesema  wamemuomba mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, kusaidiana na timu hiyo ili katika maeneo ambayo yananahusisha masuala ya jinai polisi wachukue hatua mara moja.

Aidha Waziri Mkenda ameongeza kuwa Wizara imekusudia kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa namba maalumu kwa ajili ya kutoa taarifa ya vitendo hivyo katika shule za umma au binafsi nchini.

Prof,Mkenda amesema kuwa kesho Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kesho anatatoa  namba ambayo mtu yeyote ambaye akijua kuna kitu kama hicho katika shule yeyote iwe ya umma au binafsi au vyuo vyovyote hapa nchini anaweza akapiga simu akatupa taarifa .

“Tutafatilia nchi nzima na kuongeza umakini kwa kufatilia mambo haya kwa sababu tunajua yanaweza kuchafua taswira ya elimu pamoja na kuharibu vijana wetu na hata wazazi kukosa imani na shule na Katibu Mkuu lwangu kesho atatangaza namba”amesema Prof.Mkenda

 Prof.Mkenda ameeleza kuwa  walifanya Mkutano ambao ulikuwa chini ya Mwenyekiti Waziri Simbachawene,Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk.Dorothy Gwajima,Waziri wa TAMISEMI Angela Kairuki pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo  kwa ajili ya kuangalia namna ya kudhibiti mambo hayo.

“Tumeanza mkakati wa kitaifa wa kuangalia namna ya kudhibiti mambo hayo ambayo yanatokea Mashuleni,Majumbani, Njiani na maeneo mbalimbali hivyo  siyo  suala  la Wizara moja ni suala  mtambuka  kazi inaendea na Makatibu wakuu watarudisha taarifa yao halafu tutakuwa na mkakati mzuri zaidi kitaifa.”amesisitiza

About the author

mzalendoeditor