Featured Kitaifa

ASKOFU MCHAMUNGU AWAFUNDA VIJANA,ASEMA VIJANA MAISHA YAO YANAKABILIWA NA CHANGAMOTO NYINGI KIROHO NA KIMWILI

Written by mzalendoeditor

 

Ndahani Lugunya na Angela Kibwana-Bagamoyo.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam Mhashamu Henry Mchamungu amesema kwamba,umri wa Kijana na hasa mwanafunzi una changamoto nyingi,katika maisha yake ya kila siku ndani ya jamii na mazingira anayoishi.

Alisema hayo hivi karibuni wakati akitoa Mada inayosema “Kijana na Changamoto za Sasa”,kwenye Semina iliyowajumuisha Vijana Zaidi ya 1390 katika  Kongamano la 14 Kitaifa la Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki wanaosoma Vyuo na Vyuo Vikuu nchini (TMCS) kutoka katika Majimbo mbalimbali, kwenye Viwanja vya Shule ya Wasichana ya Maria-Bagamoyo Jimboni Morogoro.

Askofu Mchamungu alisema kwamba moja ya changamoto hizo ni pamoja na masomo,kwani elimu ndio ufunguo wa maisha na hivyo kijana anahitaji kusoma ili aweze kuelimika na hatimaye kutengeneza msingi mzuri wa maisha yake ya baadae.

Aidha alisema kwamba changamoto nyingine inayowakabili vijana ni suala la ajira,kwani wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu wengi wao wanasoma wakiwa na mtazamo kwamba mara baada ya kuhitimu masomo yao wataajiriwa,lakini huwa tofauti na mtazamo wao pale wanapokuwa wamehitimu elimu yao.

“Watu wanasoma wakiwa na mtazamo kwamba baada ya masomo watapata ajira.lakini sasa hivi ndugu zangu vijana wapendwa katika nchi yetu kuna Vyuo vikuu vingi na kila mwaka maelfu na maelefu ya vijana wanahitimu na mara baada ya kuhitimu hawapati ajira.

Mtaani huko utakutana na kijana anatembea na bahasha kuomba kazi na kazi hamna.mtu anabeba bahasha yenye vyeti na wasifu kazi wake hadi bahasha inachakaa ananunua nyingine nayo inakwisha inakuwa ndiyo kazi yake kutembea na bahasha.

Sasa anaesoma anajikuta katika changamoto kama hiyo ya kuwa na mawazo kwamba anasoma lakini mbona hakuna ajira?.kwa hiyo kiasi flani inampatia mawazo kama mwanafunzi.kumbe nayo hii ni changamoto ambayo vijana wanakutana nayo  lakini msikate tamaa,” alisema Askofu Mchamungu.

Sanjari na hilo alisema kwamba matumizi ya pombe na ulevi ni changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi wanafunzi na wasio kuwa wanafunzi,kwani kutokana na ugumu wa maisha vijana wengi wamejikuta katika matumizi ya pombe kali.

“Kutokana na ugumu wa maisha vijana wengi wamekuwa wahanga katika suala zima la unywaji na ulevi na kwa sababu uwezo hawana wanaona ni bora kutumia kinywaji kile ambacho akinywa kidogo tu anajisikia kuwa amekunywa sana kwa hiyo wanatumia vinywaji vikali.

Lakini vinywaji vikali vina madhara ndugu zangu vijana,unaunguza viungo vyako vya ndani ikiwemo figo na maini yanaathirika kwa vinywaji.kwa hiyo hii ni changamoto iliyopo katika ulimwengu wa vijana kwamba sasa hivi vijana wameingia katika wimbi la kunywa vinywaji vikali” alisema Askofu Mchamungu.

Katika mada yake hiyo Askofu Mchamungu alisema kwamba  changamoto ya ugumu wa maisha kwa sasa ni chanzo kikubwa kinachofanya vijana wengi kuogopa kuingia katika Sakramenti ya ndoa.

Alisema  wapo vijana wa kiume waliofikia umri wa kuoa lakini hawaoi,vivyo hivyo vijana wa kike nao waliofikia umri wa kuolewa hawaolewi,hivyo amewataka vijana kujiwekea mikakati ya maisha ingali wapo kwenye masomo.

“Katika familia anayoishi kijana na wazazi wake wapo hai utakuta wazazi hao wanashangaa kijana umri wake unaenda lakini kama ni mvulana haoi na kama ni msichana haolewi.wazazi wake wanabaki wanashangaa na baadae anawaletea bugudha pale nyumbani kwa sababu walitazamia kwamba kijana aanze maisha yake lakini haanzi.

Sasa hii ni hali halisi ilivyo ambayo inaleta masikitiko kwa wazazi wenu.unaposoma kama kijana anza kujipangia mikakati ya maisha yako baada ya kumaliza masomo.anza kujijengea tabia nzuri ili kusudi upate mchumba mzuri na baada ya masomo basi unaamua kuanzisha familia usiende kukaa tu nyumbani hivi hivi hiyo ni hatari,” alisema Askofu Mchamungu.

Aidha alisema kwamba kuotokana na hali halisi ya maisha kuwa ngumu,kunaweza kusababisha vijana kuwa na mwelekeo wa kujiingiza katika vitendo vya kishirikina,hivyo amewataka vijana Wakristo Wakatoliki kuiishi vema Imani yao na kujiepusha na mwelekeo huo.

Pamoja na changamoto hizo,Askofu Mchamungu alisema kwamba changamoto nyingine inayowakabili vijana ni matumizi mabaya ya vyombo vya mawasiliano,ambapo kutokana na hali hiyo amewataka vijana kuvitumia vizuri vyombo hivyo ili viweze kuwa fursa kwao kimaadili na kiuchumi.

“Kuna mambo ya picha zisizofaa na kuna habari zisizofaa ambazo watu wanarushiana kwenye mitandao.kijana Mkristo mkatoliki anae muogopa Mungu na anaetaka  maisha yake ya baadaye yawe mazuri mambo ya namna hiyo ajitahidi kuyakwepa.

Kwa hiyo nawasihi vijana hivi vyombo vya mawasiliano ya jamii vitatupotosha na vitafanya maisha yetu ya baadaye yawe magumu na mabaya.kumbe ndugu wapwendwa tujitahidi kuvitumia vizuri  hivi vyombo vya mawasiliano kwa sababu ukivitumia vizuri vitakusaidia na ukivitumia vibaya maisha yako yanaharibika,kumbe tusiharibu maisha yetu kwa kuvitumia vibaya hivi vyombo vya mawasiliano,” alisisitiza Askofu Mchamungu.

Aliendelea kutaja changamoto za sasa za vijana  kuwa ni kusombwa na  mitindo (fashion) ambapo amesema,ulimwengu wa vijana umemezwa na mitindo ya maisha inayozuka kila kukicha na hivyo kupeleka vijana wengi kusombwa na mitindo hiyo hasa pale wanapokosa umakini wa kupembua mambo.

“Kijana unaweza kuvaa nguo ambayo  hata wenzako wakakushangaa.na kwa upande wa akina dada ndio wamekuwa wahanga wakubwa katika changamoto hii.yaani wakati mwingine anavaa nguo ambayo hata yeye mwenyewe anaona aibu mbele za watu kana kwamba alilazimishwa kuvaa hio nguo kumbe mtu kavaa kwa uhuru wake lakini anajikuta mbele za watu ni aibu tupu,” alisema Askofu Mchamungu.

Kutokana na hilo alitoa rai kwa vijana kutokuwa wepesi kumezwa na kubebwa na mitindo hiyo ya maisha isiyokuwa na heshima,kwani kijana ambaye ni safi kimaadili anavaa vizuri na wala hakumbwi na mitindo hiyo ya ajabu inayoibuka katika ulimwengu wa vijana.

Alisema changamoto nyingine inayowakumba vijana katika ulimwengu wa sasa ni uvivu kwa baadhi yao wakiwemo wanafunzi na wale waliohitimu elimu katika ngazi mbalimbali,kwani wapo ambao wamekuwa wakikaa vijiweni pasipo kufanya shughuli yoyote.

Askofu Mchamungu alisema vijana wamekuwa wakikusanyika katika vijiwe na kucheza michezo ya  karata,bao na kubahatisha muda ambao walipaswa wawe katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

“Kwa mtindo wa maisha ya namna hiyo huwezi kuniambia maisha yako ya baadaye yatakuwa mazuri.hayawezi kuwa mazuri hata siku moja kwa sababu hufanyi kazi na siku zote asiyefanya kazi maisha yake ya baadaye hayawezi kuwa bora.wale wanaochapa kazi ndiyo ambao hujikuta wanakuwa na maisha mazuri hapo baadaye.fanya kazi kwa bidi,” amesema Askofu Mchamungu.

Ufanyaji wa biashara haramu ni miongoni mwa changamoto ambayo imetajwa na Askofu Mchamungu,ambapo alisema kwamba kwa sasa ufanyaje wa biashara haramu kumeshamiri hususani kwa vijana akitolea mfano uuzaji wa madawa ya kulevya.

Alisema kutokana na ugumu wa maisha vijana ambao wamehitimu masomo baadhi yao wamejikuta wametumbukia katika changamoto hiyo ya ufanyaji wa biashara haramu,kwa sababu ya matamanio ya kupata fedha kwa haraka,kumbe vijana wajihadhari na wimbi hilo na kamwe wasikubali kudanganywa na mtu kuingia katika biashara hiyo.

Pamoja na kufanya biashara  hiyo haramu ya uuzaji wa madawa ya kulevya wapo pia wengine wamekuwa wahanga wa kutumia madawa hayo,na kupeleka kuharibu ndoto za maisha yao na kuleta hasara kwa familia,jamii inayo wazunguka na Taifa zima kwa ujumla.

Aidha alisema kutokana na ugumu wa maisha baadhi ya vijana na hasa akina dada wamejiingiza katika biashara haramu ya kujiuza miili yao  kwa ajili ya kujipatia fedha za haraka,jambo ambalo ni hatari kwao kwani kuna uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa.

Askofu Mchamungu alisema madhara mengine ya tabia hiyo chafu ya kujiuuza miili kwa wasichana ni kukosa uaminifu pale ambao kijana anaingia katika wito ndoa, kutokana na mazoea aliyojijengea ya kukutana na wanaume wengi na tofauti.

Sanjari na changamoto hizo Askofu Mchamungu alisema ushoga na usagaji ni miongoni mwa changamoto nyingine ambayo kwa sasa inashamiri kwa kasi kubwa  miongoni mwa vijana,ambapo amesema zipo baadhi ya nchi zilizoendelea zinatumia fedha kwa vijana ili kuendeleza tabia hiyo chafu.

Alisema kwa bahati mbaya zaidi tabia hiyo imeendelea kukithiri hata katika shule hasa zile za bweni zenye wanafunzi wavulana pekee na wasichana pekee,hivyo amesema tabia inapaswa kupingwa na kukemewa na kila mtu kwani isipo kemewa matokeo yake yatakuwa ni mabaya katika Taifa na kwa Kanisa pia.

“Vijana wapendwa nawasihi na kuwaomba mjiupushe na hilo.kamwe msivutiwe na tamaa za hao wanaomwaga  fedha ili kusambaza tabia chafu za namna hiyo.msikubali na kataeni tena kwa ukali kabisa,” alisema Askofu Mchamungu.

Askofu Mchamungu alihitimisha mada yake ya  “Kijana na changamoto za Sasa”  kwa kuwaalika vijana kumuwekea matumaini  yao Mwenyezi Mungu,hatimaye waweze kupata faraja,ili changamoto wanazokutana nazo kama vijana ziwe nyepesi kuzitatua.

About the author

mzalendoeditor