Featured Kitaifa

WIZARA YA ELIMU NA TAASISI ZAKE ZAKUTANA KUTATHMINI UTEKELEZAJI WA MALENGO

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara kukutana kila robo mwaka kufanya tathmini ya pamoja ya utekelezaji wa malengo.

Agizo hilo limetolewa leo tarehe 14 Desemba, 2022 jijini Dar es salaam katika kikao kati ya Wizara na Taasi zake kilicholenga kutathmini utekelezaji wa malengo ya robo mwaka mbili zinazoishia Desemba 2022.

“Kikao hiki kimetuleta pamoja Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ambao ni watekelezaji wakuu wa miongozo, Sera na Mipango tunayojiwekea ili kufikia malengo yakiwemo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa na Ilani ya CCM”, amesema
Dkt. FrancisMichael

Katibu Mkuu ameongeza kuwa ameaona ni vema kuanzisha utaratibu wa kuwa na tathmini ya pamoja ili kutambua mafanikio ya malengo yetu, changamoto tunazokutana nazo ili kwa pamoja tuone wapi tuongeze kasi na kuweka uelekeo.

Amezitaka Taasisi pia kushirikisha wadau wakati wa kuandaa mipango ili kujua mahitaji halisi katika Sekta. Amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kuwa na mipango sahihi ya kutekeleza katika mwaka.

Katibu Mkuu Michael amepongeza Taasisi kwa kuendelea kutekeleza majukumu kwa ubunifu na kuwataka kuongeza kasi za kuja na mbinu za kibunifu zaidi ili kufikia malengo mapana ya kitaifa.

Katika hatua nyingine Dkt. Michael amewaagiza Taasisi kutangaza kazi kubwa zinazofanyika katika maeneo yao ya kazi kwani wananchi wana ari kubwa ya kusikia mafanikio hayo na si kujibu malalamiko tu.

“Fanyeni kazi na vyombo vya habari na tukifanya kitu kizuri tutangaze na kama kiongozi huwezi mwambie afisa habari aseme,” ameeleza Dkt. Michael

Kwa upande wake Abdul-Razaq Badru Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ameipongeza Wizara kwa kuja na mpango huo ambao amesema utasaidia katika kubadilishana uzoefu kutatua changamoto kwa pamoja na kupanga mikakati kwa pamoja kujenga timu ili kwa pamoja hatimae kufikia malengo mapana ya sekta.

Nae Dkt Mboni Ruzegea Mkurugenzi Mkuu wa Bodi Huduma za Maktaba amemshukuru Katibu Mkuu kwa hatua ya kuanzisha vikao hivi na kuahidi kuendelea kuimarisha mikakati ya kutangaza mafanikio na fursa mbalimbali zilizoko katika taasisi.

About the author

mzalendoeditor