Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU AZINDUA KIWANDA CHA KUCHAKATA MAZIWA NSIMBO

Written by mzalendoeditor

 

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua kiwanda cha maziwa cha MSS Fresh Milk katika jimbo la Nsimbi Mkoani Katavi akiwa katika ziara ya mkoa huo, Disemba 13, 2022. Wa  tatu kulia ni Mkurugenzi wa kiwandanda hicho Salum Maliki, wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Katavi  na Mkuu wa wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu na kushoto ni Mbunge wa Nsimbo, Anna Lupembe. 

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa kiwanda cha maziwa cha MSS Fresh Milk cha Nsimbo, Salum Maliki (kushoto)  kuhusu maziwa yanayozalishwa kiwandani hapo baada ya kuzindua kiranda hicho, Disemba 13,  2022.  Kulia ni Mbunge wa Nsimbo, Anna Lupembe.  

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati  alipozindua kiwanda cha maziwa cha MSS Fresh Milk katika jimbo la Nsimbi Mkoani Katavi akiwa katika  ziara ya mkoa huo, Disemba 13, 2022.  Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa kiwanda, Salum Maliki, wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, kulia ni Naibu Waziri  Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, wa pili kulia ni Mbunge wa Nsimbo, Anna Lupembe. Wa pili kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa atavi na Mkuu wa Wilaya ya Tanganiyika, Onesmo Buswelu na kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Katavi,  Iddi Kimanta.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Salum Maliki ambaye ni  Mkurugenzi wa kiwanda cha maziwa cha MSS Fresh Milik  cha Nsimbo Katavi  kuhusu uzalishaji maziwa katika kiwanda hicho baada ya kukizindua akiwa katika ziara ya mkoa wa Katavi Disemba 13, 2022. Kulia ni Mbunge wa Nsimbo, Anna Lupembe.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Naibu Mawaziri, Wabunge na wafanyakazi wa kiwanda cha maziwa cha MSS Fresh Milk cha Nsimbo Mkoani Katavi baada ya kuzindua kiwanda hicho, Disemba 13, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…………………………

* Kiwanda hicho kina uwezo wa kusindika wastani wa lita 10,000 kwa saa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua kiwanda cha kuchakata maziwa cha MSS kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mkoani Katavi ambacho kina uwezo wa kusindika wastani wa lita 10,000 kwa saa.

Akizungumza baada ya kuzindua kiwanda hicho ambacho uwekezaji wake umegharimu shilingi milioni 600, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili kila mwenye uwezo awekeze.

Amesema hayo leo {Desemba 13, 2022} wakati akizungumza na wananchi baada ya kuzindua kiwanda hicho ambacho kwa sasa kinazalisha maziwa ya mtindi na maziwa fresh na kinatarajia kuanza uzalishaji wa Samli hivi karibuni.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa rai kwa wafugaji wanaozunguka kiwanda hicho kuuza maziwa kwa mwekezaji huyo ili waweze kujiongezea kipato na kumwezesha mwekezaji huyo kuwa na uhakika wa malighafi ya kutosha.

“Huyu Bwana Maliki anamuunga mkono Rais Mheshimiwa Dkt. Samia katika nia yake ya kuendeleza uwekezaji nchini. Uwepo wa kiwanda hiki kunaisaidia kuendeleza  mkakati wa lishe bora kwa kila Mtanzania, kwa sasa tunamshauri aendelee kupanua kiwanda hiki ili aongeze uzalishaji na wananchi wengi wazidi kupata ajira.”

Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi inayojengwa katika eneo la Ilembo, Mpanda, ambapo alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya sita imeendelea na mkakati wa kupeleka huduma karibu na wananchi kwa kuhakikisha inajenga majengo ya ofisi ya mikoa na wilaya mpya  Katavi ukiwemo.

Aidha,alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kwamba Serikali yao itaendelea kuwatumikia, hivyo waendelee kuiamini na kuiunga mkono. “Serikali itaendelea kuwatumikia na haitowaangusha sisi wasaidizi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia tutafanya kazi wakati wote, wakati wa jua kali na hata wakati wa mvua, tunataka kuhakikisha dhamira ya Rais wetu ya kuleta maendeleo inatimia.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema kuwa Rais Dkt. Samia ameridhia kutoa shilingi milioni 200 kupitia Bodi ya Maziwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha ukusanyaji wa maziwa Mpanda, Katavi. “Vituo hivi vitajengwa takribani kumi nchi nzima na kila kimoja kitagharimu shilingi milioni 200.”

Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia ametoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitamba ya maziwa 500 na madume ya nyama 500 ambayo yatagawiwa nchi nzima, lengo likiwa ni kuboresha aina ya mifugo inayofugwa na wananchi. “Serikali inataka wananchi wafuge kisasa na kibiashara.”

Naye, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini {DPP} kufanya mapitio ya kesi na  majalada mbalimbali ili yasiyokuwa na mashiko au ushahidi wa kutosha yaondolewa ili wahusika  wakaendelee na shughuli za uzalishaji mali.

 

About the author

mzalendoeditor