Featured Kitaifa

WAZIRI JAFO ATAKA MAJENGO YAWEKWE MFUMO WA MAJI YA MVUA

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akitoa maelekezo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma

Jengo la jengo jipya la Ofisi ya Makamu wa Rais likiwa katika hatua ya ujenzi katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo Desemba 13, 2022 ambapo lililaguliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo.

(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

…………………………….

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameelekeza majengo yote ya Serikali yanayojengwa katika eneo la Mtumba jijini Dodoma kuwekwa amfumo wa kuvuna maji ya mvua kuepusha athari za kimazingira.

Ametoa maelekezo hayo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo Desemba 13, 2022. 

Amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo ikiwemo utekelezaji wa maelekezo ya kuweka mifumo ya uvunaji maji aliyotoa alipokagua ujenzi huo mwezi Juni mwaka huu. 

Dkt. Jafo amesema kuwa kujengwa kwa mifumo ya kuvuna maji ya mvua kutasaidia yasiweze kutiririka ovyo na kusababisha mmomonyoko wa udongo hivyo kuharibu mazingira. 

“Kwa kweli nimefarijika sana na mnavyoendelea na utekelezaji wa mradi huu wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais nilipofanya ziara hapa nilitoa maelekezo na nimekuta mnayatekeleza maana mmejenga tanki hili la lita laki tano litakapokea maji ya mvua,” alisema Dkt. Jafo.

Aidha, Waziri Jafo alitoa rai kwa mkandarasi anayejenga jengo hilo kumaliza kazi zilizobakia kwa wakati ili jengo hilo liweze kukamilika ndani ya muda uliobaki.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo Mhandisi wa SUMA JKT Sajidu Bwikizo alisema ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 50 kwa mujibu wa mpango ambapo umefikia hatua ya usukaji wa nondo na umwagaji wa zege hadi sakafu (floor) ya sita.

Pia, Msimamizi wa Mradi Meja Benedict Meela aliahidi kuyafanyia kazi maelezo ya waziri kwa kuweka mafundi wa kutosha katika kila sakafu ili kazi hiyo ifanyike na kukamilika kwa wakati. 

Ikumbukwe kuwa ujenzi wa jengo hilo unasimamiwa na Mshauri Elelekzi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kutekelezwa na Mkandarasi SUMA JKT.

About the author

mzalendoeditor