Mkataba wa upanuzi wa mfumo wa majita ukisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (kushoto) na Katibu Mtendaji wa LVBC, Dkt. Masinde Bwire (kulia). Wanaoshuhudia ni viongozi wa Wizara ya Maji na MWAUWASA.
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (kushoto) akibadilishana mkataba na Katibu Mtendaji wa LVBC, Dkt. Masinde Bwire mara baada ya kusaini.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Charles Mafie (kushoto) akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa upanuzi wa mfumo wa majitaka
Wawakilishi wa LVBC, Wizara ya Maji, Bodi na Menejimenti ya MWAUWASA mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa upanuzi wa mfumo wa majitaka.
……………………….
Na Mohamed Saif
Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imesaini mkataba wa shilingi bilioni 12.7 na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (‘LVBC’) kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa majitaka utakaonufaisha wakazi 7,360 Jijini Mwanza.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Charles Mafie akimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga kwenye hafla ya utiaji saini Novemba 23, 2022 alipongeza jitihada za LVBC kwenye utunzaji wa Ziwa Victoria.
Mhandisi Mafie alisema wananchi wanahitaji maji safi na salama na kwamba jitihada za makusudi za utunzaji wa vyanzo vya maji zisipofanyika, maji salama hayotapatikana.
“Kwa mkataba huu na program hii kwa Mwanza tunakwenda kuhakikisha kwamba Ziwa Victoria linakwenda kulindwa na sio suala la maji pekee kwani Ziwa likichafuka maana yake hata samaki hatutapata kwahiyo hapa tunazungumzia suala la lishe pia,” amesema Mhandisi Mafie.
Hata hivyo aliisisitiza LVBC kutazama namna ya kutanua program hiyo na kuifikisha kwenye miji mingine inayozunguka Ziwa Victoria ikiwemo mji wa Musoma na Bukoba ili kusiwe na uchafuzi kutoka kwenye maeneo yote yanayozunguka Ziwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele amebainisha kuwa utanufaisha wakazi wa Kata za Igogo, Kitangiri, Kirumba, Pasiansi na Nyamanoro.
Amebainisha kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha maji ya Ziwa Victoria yanaendelea kuwa salama na kwamba jitihada, mikakati na hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na uwepo wa mradi huo.
“Tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kutuletea mradi huu, sisi pia kama taasisi tutanufaika kwani kulinda uchafuzi wa Ziwa maana itasaidia kupunguza gharama ya kutibu maji kabla ya kuyapeleka kwa wananchi,” amesema Mhandisi Msenyele.
Mhandisi Msenyele ameihakikishia Serikali kuwa MWAUWASA itasimamia vyema utekelezaji wa mradi na kwamba kila kipengele kwenye mkataba kitasimamiwa kwa weledi na kwa kuzingatia miiko ya kitaaluma ili kuleta tija iliyokusudiwa.
“Serikali kupitia Wizara ya Maji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Fedha na Mipango imetuamini kusimamia mradi huu, tunaahidi kutekeleza kwa uaminifu mkubwa ili manufaa yaliyokusudiwa yapatikane,” amesema Mhandisi Msenyele.
Naye Katibu Mtendaji, Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Dkt. Masinde Bwire amesema chimbuko la mradi unatokana na mradi wa kwanza wa Uhifadhi wa Mazingira ya Ziwa Victoria (‘LVEMP’) ambao haukuweza kutatua changamoto zote kwa wakati huo ikiwemo ya uchafuzi wa Ziwa.
“Mradi huu umeainisha changamoto zilizoshindwa kutatuliwa na mradi wa kwanza (LVEMP) kwani hadi sasa uchafuzi wa Ziwa Victoria bado ni mkubwa kutoka kwenye miji inayozunguka ikiwemo Mwanza, Kampala, Kisumu, Musoma na Bukoba,” anabainisha Dkt. Bwire.
Amesema jukumu kubwa la LVBC ni kusimamia matumizi endelevu ya Rasilimali za Maji na rasilimali zingine ndani ya ukanda wa Ziwa Victoria na kwamba ni wajibu wao kutafuta fedha kwa kushirikiana na Serikali za Jumuia sambamba na wadau wa mazingira na maendeleo.
“Kwa sasa tumefanikiwa kupata kiasi cha shilingi za Kitanzania Bilioni 12.7 kwa ajili ya mradi huu ambao unatekelezwa kupitia Mpango Jumuishi wa Usimamizi wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Ziwa Victoria (‘LVB IWRMP’) na usimamizi wake utakuwa chini ya MWAUWASA,” amesema Dkt. Bwire
Amesema utakamilika mwishoni mwa Mwaka 2025 na kwamba jitihada za kutafuta fedha zaidi kutoka kwa wadau zinaendelea kwani uchafuzi wa Ziwa Victoria bado ni mkubwa.
“Rai yetu kwa Mamlaka za Miji inayozunguka Ziwa Victoria ni kuendelea kuhimiza usafi wa mazingira na kufanya matumizi endelevu ya Rasilimali za Maji na vyanzo vya maji,” amesisitiza Dkt. Bwire.