Featured Kitaifa

VIONGOZI NA WATUMISHI WAPEWA MAFUNZO KUHUSU MASUALA YA PROTOKALI

Written by mzalendoeditor

KATIKA  kuimarisha utendaji Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatoa mafunzo kwa viongozi na watumishi juu ya masuala ya Protokali kwa lengo la kuwajengea uwezo.

Akifungua mafunzo hayo jijini Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Francis Michael amewataka viongozi na watumishi hao kuhakiksha wanashiriki kikamilifu ili matokeo ya mafunzo hayo yaweze kuonekana katika utendaji.

“Nimezisikia mada ambazo mtakwenda kufundishwa zote ni muhimu na zina tija katika kuimarisha utendaji na utoaji huduma kwa wateja ndani na nje ya wizara, hakikisheni mnashiriki kikamilifu,”amesema Dkt. Michael

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Moshi Kabengwe amesema mafunzo hayo yamejumuisha washiriki 147 ambao ni Wakurugenzi, Wakurugenzi Wasaidizi, Wakuu wa Idara na Vitengo, Makatibu Mahsusi, Watunza Kumbukumbu na baadhi ya Wathibiti Ubora wa Kanda na Wilaya.

Ametaja mada zitakazowasilishwa katika kikao hicho kuwa ni masuala ya Itifaki, Mawasiliano fanisi ndani na nje ya Wizara, Misingi ya utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka pamoja na Utendaji wa pamoja (team work).

About the author

mzalendoeditor