KAIMU Katibu Msaidizi Kanda ya Kati –Dodoma Bi. Modesta Mtui,akizungumza wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa walezi wa klabu za maadili kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma .Kushoto kwake ni Afisa uchunguzi Sekretarieti ya Maadili Bw. Anno Mgani na kulia kwa Kaimu Katibu ni Afisa Uchunguzi Sekretarieti ya Maadili Bi. Philipina Kobelo yaliyofanyika leo Oktoba 28,2022 jijini Dodoma.
…………………..
Kaimu Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya kati Dodoma Bi. Modesta Mtui,amewaasa walezi wa klabu za maadili kuwa na maadili mema katika jamii inayowazunguka.
Hayo ameyasema leo Oktoba 28,2022 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya walezi wa klabu za maadili kwa shule za Sekondari na Msingi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma .
Bi. Mtui alisema kuwa walezi wa klabu za maaadili wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwa na maadili mema kwani mtoto anachokiona ndicho atakachokiishi hivyo mwalimu yeyote ni kioo kwa wanafunzi wake “Ni ngumu sana kwa mwalimu ambaye hana maadili kumfundisha mwanafunzi kuwa na maadili mema na mwanafunzi akaelewa’’’alisema.
Bi. Modesta alisema kuwa lengo la mafunzo hayo kwa walezi wa klabu hizo ni kupata uelewa wa pamoja juu ya dhana pana ya maadili ili walezi hao wa klabu za maadili wawasaidie wanafunzi kuyaishi yale wanayofundishwa jambo litakalowasaidia kuwa waadilifu toka utotoni hata watakapokua wakubwa.
Bi. Modesta alieleza kuwa Serikali kupitia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambacho ndio chombo kikuu cha usimamizi wa maadili ya Viongozi nchini , iliona ni vyema kueneza maadili kwa wanafunzi walioko ngazi mbalimbali za masomo kama vile shule za msingi , sekondari pamoja na vyuo vikuu kwa kuanzisha klabu za maadili ikiaminika kuwa tabia na mienendo mwema kwa binadamu hufundishwa tangu akiwa mdogo na hasa akiwa shuleni au chuoni.
Aidha Bi. Modesta alisema kuwa Lengo la kuanzishwa kwa klabu za maadili ni kuwajengea wanafunzi na wanavyuo misingi bora ya maadili tangu wakiwa shuleni na vyuoni. Klabu hizo pia zitasaidia kuwatengeneza mabalozi wazuri wa Sekretarieti ya Maadili watakaosaidia kueneza na kuelimisha familia zao kwa ujumla juu ya suala la maadili. Klabu hizo pia zitawasaidia wanafunzi kujitambua na kujipambanua kitabia na kuachana na mienendo isiyofaa.
Akibainisha changamoto wanazokutana nazo walezi wa klabu za maadili ambao ni waalimu wa shule mbalimbali Mwalimu Marcus Magwa ambaye ni mlezi wa klabu ya maadili katika shule ya sekondari Dodoma alisema kuwa kutokana na kukua kwa utandawazi kwa sasa watoto wengi wanapata misukumo ya mienendo mibaya kutoka kwenye mitandao jambo linalowafanya watoto hao kuona kuwa kuwa na maadili ni ushamba mfano katika suala la mavazi mtoto anaona kuvaa nguo zinazomstiri mwili wake ni jambo lililopitwa na wakati.
Aidha Mwalimu Marcus alitoa wito kwa wazazi kutenga muda wa kukaa na watoto wao na kufuatilia mienendo yao ili kuweza kubaini mapema iwapo mtoto ana mienendo isiyofaa ili washirikiane na waalimu kuweza kudhibiti hali hiyo mapema .
Pamoja na hayo Mwalimu Marcus alitoa rai kwa Sekretarieti ya Maadili kuongeza kasi ya kueneza maadili nchini hususan kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wanachama wa klabu ya maadili ili kuendana na kasi ya ukuaji wa utandawazi nchini ’’ utandawazi una nguvu unakua kwa kasi sana’’ alisema.
Katika mafunzo hayo walezi wa klabu za maadili watapata uelewa wa pamoja juu ya shughuli zinazotekelezwa na Sekretarieti ya maadili, majukumu ya Sekretarieti ya Maadili .Katika mafunzo hayo walezi wa klabu za maadili watapata fursa ya kupitia mwongozo wa kuanzisha na kuendesha klabu za maadili katika shule za msingi, Sekondari na Vyuo vya elimu Tanzania na kutoa maoni yao juu ya namna bora ya utekelezaji wa mwongozo huo.
KAIMU Katibu Msaidizi Kanda ya Kati Dodoma Bi. Modesta Mtui,akizungumza wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa walezi wa klabu za maadili kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma .Kushoto kwake ni Afisa uchunguzi Sekretarieti ya Maadili Bw. Anno Mgani na kulia kwa Kaimu Katibu ni Afisa Uchunguzi Sekretarieti ya Maadili Bi. Philipina Kobelo yaliyofanyika leo Oktoba 28,2022 jijini Dodoma.
KAIMU Katibu Msaidizi Kanda ya Kati Dodoma Bi. Modesta Mtui,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua mafunzo ya maadili kwa walezi wa klabu za maadili kutoka shule mbalimbali za msingi na sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma yaliyofanyika leo Oktoba 28,2022 jijini Dodoma.