Featured Michezo

MCHEZO WA DRAFTI WAIPA UKAKASI TIMU YA TAMISEMI

Written by mzalendoeditor

Na. Asila Twaha, Tanga

Katika Mashindano ya Michezo ya Shirikisho ya Wizara, Idara za Serikali na Mikoa( SHIMIWI) yanayoendelea Tanga katika mchezo drafti umeipa ukakasi wa sintofahamu timu ya TAMISEMI.

Katika mchezo uliochezwa Oktoba 12, 2022 katika ukumbi wa Police Mess kumetokea sintofahamu katika ratiba ambapo mchezaji wa timu ya TAMISEMI B2 alitakiwa kucheza na mshindi wa kwanza wa kundi G1.

Katibu wa TAMISEMI Sports Club Bw. Alex Morice amesema, katika mchezo wa makundi wachezaji wawili akiwemo wa TAMISEMI walilingana kwa pointi 9 hivyo ikachezwa mechi moja kuamua mshindi wa kwanza na wa pili.

Aliendelea kueleza kuwa, mchezaji wa TAMISEMI alishindwa katika mchezo huo na kushika nafasi ya pili katika kundi B, hivyo kuingia katika hatua ya 16 bora.

“Katika hatua ya 16 bora TAMISEMI ilitakiwa kucheza na mshindi wa kwanza wa kundi G lakini taarifa za waamuzi zilisema sisi tumekuwa wa kwanza kundi B hivyo tunatakiwa kucheza na mshindi wa pili G2 ambapo haikuwa sahihi” amesema Morice

Kwa upande wa mchezaji wa TAMISEMI Vicky Zayumba amesema, amesikitishwa kwa namna matokeo yake yalivyobadilishwa.

“Ningepangiwa kucheza na mtu sahihi kama mchoro ulivyokuwa naamini ningefanya vizuri zaidi lakini kwa namna matokeo yangu yalivyobadilishwa inavunja moyo washiriki” ni dhahiri kuna mtu alikuwa anatengenezewa njia nyepesi” amesema Zayumba.

Akiongeza Katibu wa Timu ya TAMISEMI Bw. Alex Morice amesema ni vizuri michezo ifuate taratibu, kanuni na sheria za michezo.

“Ili kuwe na imani kwa washiriki, viongozi tumepewa dhamana ya usimamizi ni imani yetu michezo hii iendeshwe kwa haki ili kusiwe na ukakasi na washindi wapatikane kwa haki”

Kwa hatua ya mchezo wa drafti uliochezwa jana na kupatikana kwa mshindi wa kwanza TAMISEMI ilitolewa katika hatua ya robo fainali.

About the author

mzalendoeditor