Featured Kitaifa

VIONGOZI WA UMMA WAASWA KUWA MSTARI WA MBELE KWA KUFANYA KAZI KWA UADILIFU.

Written by mzalendoeditor

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi,akizungumza wakati akifungua mafunzo ya Maadili yaliyotolewa kwa Viongozi mbalimbali wa Umma yalifanyika leo Oktoba 13,2022 Jijini Dar es Salaam.

………………

Viongozi wa Umma wanategemewa kuwa mstari wa mbele katika kuzingatia na kutekeleza majukumu ya umma kwa uadilifu ikiwa ni pamoja na kusimamia na kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Hayo yalisemwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi wakati akifungua mafunzo  kuhusu ya Maadili yaliyotolewa kwa Viongozi mbalimbali wa Umma. Mafunzo hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Ofisi ndogo ya Bunge Jijini Dar es Salaam.

Akifungua mafunzo hayo Mhe. Mwangesi alisema kuwa jitihada za Serikali kupitia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoa mafunzo hayo kwa Viongozi ni kielelezo dhahiri kuwa Serikali ya awamu ya Sita imedhamiria kuhakikisha kuwa suala la maadili ya uongozi linaeleweka kwa wadau wote wa sekta ya Umma na sekta binafsi.

Mhe. Mwangesi alisema kuwa Tanzania inahitaji Viongozi ambao ni mfano mzuri wa uzingatiaji  wa maadili, Viongozi wanaozingatia Sheria, Kanuni na taratibu katika utendaji wao wa kazi, Viongozi wanaotumia nafasi zao za uongozi kwa kuwaletea wananchi maendeleo na si kwa maslahi yao binafsi jambo ambalo litawafanya wananchi kuwa na imani kwa viongozi wanaowaongoza na Serikali yao kwa ujumla. “Uongozi ni dhamana  hivyo kiongozi yeyote anatakiwa atumie wadhifa wake kwa manufaa ya wananchi na si kwa manufaa yake binafsi’’alisema.

Aidha, Mhe. Mwangesi alieleza kuwa ukuzaji wa maadili kwa viongozi wa umma nchini ni moja ya jitihada za kuhakikisha kuwa malengo ya Dira ya Taifa yanafikiwa kama yalivyopangwa “kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa katika kipengele cha Utawala Bora inatarajiwa kwamba ifikapo mwaka 2025 uadilifu unapaswa kuwa sehemu ya utamaduni wa jamii ya Tanzania na hilo linawezekana ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake’’alisema. 

Mhe.Mwangesi aliendelea kusema kuwa katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo, Serikali  imedhamiria kujenga utumishi wa umma ulio imara ambao utakuwa muhimili mkuu wa kujenga uchumi bora na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi “Nitoe rai kwenu Viongozi kuwa mafunzo haya yawe chachu ya kuongeza kasi ya kujenga na kukuza maadili kati yetu ili tuweze kutoa huduma bora kwa wananchi’’ alisema.

Pamoja na hayo Mhe. Mwangesi aliwakumbusha Viongozi wa Umma kuhusu misingi ya maadili ambayo ni pamoja na Kiongozi wa Umma kutoa matamko mbalimbali ikiwemo Tamko la Rasilimali, Maslah na Madeni, kutotumia vibaya rasilimali za umma, kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, uaminifu, uwazi, haki na kutopendelea pamoja na misingi minginemingi kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. “Kama kila kiongozi ataamua kufuata misingi hii basi rasilimali za nchi yetu zitakua salama na wanannchi watakua na imani kubwa kwa Serikali yao” alisema.

Mhe. Mwangesi alimaliza kwa kusema kuwa pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali ya kukuza maadili nchini ni muhimu jamii ikatambua kuwa vita dhidi ya ukiukwaji wa maadili siyo la Serikali pekee bali ni jukumu la jamii nzima, kuanzia mtu mmoja mmoja, katika ngazi ya familia, taasisi mbalimbali za kidini, sekta binafsi, asasi zisizo za kiraia pamoja na taasisi nyingine nyingi. 

Katika mafunzo hayo ya siku moja mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwa ni pamoja na mada kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, mada kuhusu uwajibikaji wa pamoja, Kanuni za Mgongano wa Maslah, Kanuni za Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma na mada kuhusu Tamko la Rasilimali na Madeni.

Mada hizo  zitawajengea Viongozi uwezo wa kuifahamu zaidi Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kanuni zake jambo litakalowasaidia kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa uadilifu mkubwa.

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi,akizungumza wakati akifungua mafunzo ya Maadili yaliyotolewa kwa Viongozi mbalimbali wa Umma yalifanyika leo Oktoba 13,2022 Jijini Dar es Salaam.

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua  mafunzo ya Maadili yaliyotolewa kwa Viongozi mbalimbali wa Umma yalifanyika leo Oktoba 13,2022 Jijini Dar es Salaam.

About the author

mzalendoeditor