Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (kulia), akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Barabara wa Sekta ya Ujenzi, Eng. Aloyce Matei (katikati) na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya, Eng. Matari Masige (kushoto) mara baada kukagua hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara kuu iendayo Zambia (TANZAM Highway) eneo la Inyala, Mkoani Mbeya.
……………………………….
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amemuagiza Katibu Mkuu wa Ujenzi, Balozi Aisha Amour, kupeleka kiasi cha shilingi Bilioni mbili katika ofisi ya Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mbeya ili kusaidia kuboresha barabara katika eneo la Inyala ambapo kumekuwa na mfululizo wa ajali za mara kwa mara.
Ametoa agizo hilo mkoani Mbeya, mara baada ya kukagua eneo la Mlima Nyoka hadi Mteremko wa Shamwengo ambapo pamoja na mambo mengine Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa fedha hizo zifike haraka kwani mkandarasi ameshapatikana na kuanza kazi za awali za maboresho ya eneo hilo zinaendelea ili kukamilisha ujenzi wa barabara ya mchepuo km 2.8 kwa kiwango cha lami pamoja na uwekaji wa taa za barabarani.
“Eneo hili limekuwa na changamoto za ajali za mara kwa mara hivyo,nimeamua kuja kukagua hapa ili kushuhuhudia kazi zinazoendelea kufanyika, ni imani yangu kuwa kukamilika kwa kazi hii kutapunguza changamoto za ajali na magari yataendelea kupita bila kupata changamoto zozote”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amebainisha mipango ya muda mfupi iliyochukuliwa ili kupunguza ajali katika eneo hilo ni pamoja na kujenga sehemu za kuegesha magari ili kuwapa nafasi Jeshi la Polisi kufanya ukaguzi wa magari ya masafa marefu kabla ya kuyaruhusu kuendelea na safari pindi wanapokaribia kupita eneo la Inyala na kuongeza idadi ya alama za tahadhari katika kuimarisha usalama wa eneo hilo.
Ametaja kazi nyingine zinazoendelea ni matengenezo ya barabara ya mchepuo yenye urefu wa KM 2.8 kwa kiwango cha changarawe kama sehemu ya kuyachepusha magari ya abiria na madogo ili yasichangamane na magari makubwa wakati wanateremka katika mlima huo mkali.
Aidha, Waziri huyo amebainisha mipango ya muda mrefu ambayo Serikali imejiwekea ni kupanua barabara hiyo na kuwa njia nne kutoka Igawa – Tunduma yenye urefu wa kilometa 218 ili iweze kukidhi mahitaji ya sasa.
“Barabara hii ilijengwa mwaka 1968 hadi 1973 na kufanyiwa ukarabati mkubwa mwaka 1993 na sasa Serikali inaendelea kuiboresha kuwa ya kisasa na ubora ili kuruhusu magari makubwa na madogo kupita bila ya changamoto zozote”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera, amemshukuru Waziri huyo kwa kukagua na kujionea kazi inavyoendelea na amemuahidi kutoa ushirikiano kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama na wananchi katika ulindaji na uhakikishaji wa usalama wa watu, mizigo na mali wakati wote.
Awali akitoa taarifa Meneja wa TANROADS, mkoa wa Mbeya, Eng. Matari Masige, amemueleza Waziri huyo kuwa hivi sasa wanafanya upanuzi wa barabara hiyo kwa kuongeza urefu kutoka mita 6.7 hadi kufikia mita 10.5 ili kuruhusu magari matatu kupishana kwa wakati mmoja bila ya kusababisha madhara.
“TANROADS inaendelea na uboreshaji wa upana wa barabara kwa kuongeza urefu hadi kufikia mita 10.5 ili magari mawili yakiwa yanapanda na moja linashuka na kama kuna shida yoyote imetokea basi kusiifunge hiyo barabara”, amefafanua Eng. Masige.
Hatua za maboresho ya barabara kuu iendayo Zambia (TANZAM Highway), eneo la Inyala zimetokana changamoto ya wingi wa ajali zilizokuwa zikitokea na kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo, majeruhi na upotevu wa mali kwa watumiaji wa barabara hiyo kuanzia mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (kulia), akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Barabara wa Sekta ya Ujenzi, Eng. Aloyce Matei (katikati) na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya, Eng. Matari Masige (kushoto) mara baada kukagua hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara kuu iendayo Zambia (TANZAM Highway) eneo la Inyala, Mkoani Mbeya.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (katikati), akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera, kuhusu hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Mkoa kwa eneo la Inyala wakati Waziri huyo alipokagua maendeleo yake Mkoani Mbeya. Kulia ni Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya, Eng. Matari Masige.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akizungumza na wananchi wa Kata ya Shamwengo, wilaya ya Mbeya Vijijini (hawapo pichani) wakati alipokagua maendeleo maendeleo ya ujenzi wa barabara kuu iendayo Zambia (TANZAM Highway) eneo la Inyala Mkoani Mbeya.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (kulia), akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera, wakati wa ukaguzi wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara kuu iendayo Zambia (TANZAM Highway), eneo la Inyala, Mkoani Mbeya.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia), akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya, Eng. Matari Masige, kuhusu hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara kuu iendayo Zambia (TANZAM Highway), eneo la Inyala wakati Waziri huyo alipokagua maendeleo yake Mkoani Mbeya. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera.
Muonekano wa sehemu ya barabara kuu iendayo Zambia (TANZAM Highway) ambayo kwa sasa inaongezwa upana kutoka mita 6.7 hadi 10.5 ili kuruhusu magari kupishana kwa urahisi Mkoani Mbeya.
PICHA NA WUU