Na Ndahani Lugunya,Dodoma.
Ili kuhakikisha mtoto analelewa vema kiroho na kimwili,imeelezwa kwamba zipo hatua mbalimbali ambazo zinatakiwa kufuatwa na mzazi au mlezi, ikiwa ni pamoja na kumlea katika hekima na busara ili akuwe katika maadili mema.
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA) Dekania ya Mt.Petro Mtume na Katibu wa UWAKA Parokia ya Mt.Petro Mtume-Swaswa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma,Bw. Peter Mhagwa ,wakati akizungumza na MZALENDO BLOG kuhusu Malezi ya Wazazi kwa watoto.
Mhagwa alisema kuwa mtoto anapolelewa katika maadili mema inamsaidia kuishi vema na jamii inayomzungumka kwa wakati uliopo na wa baadaye,na hata pale anapokuwa Kiongozi katika Jamii au Kanisa ataendelea kuwa Kiongozi mwenye maadili mema.
“Lakini wajibu mwingine ni kumlinda mtoto katika hatari zote za kiroho na za kimwili huo ni wajibu mkubwa wa mzazi, kwa sababu mtoto anapokuwa anaendelea kukua yeye wakati mwingine anakua hajui hatari anazozipitia lakini wewe kama mzazi unazijua hatari mtoto anazoweza kupitia.”amesema
Pia ametaja wajibu mwingine wa mzazi ni kumpa mtoto haki zake za msingi stahiki ikiwemo elimu na afya lakini pia kumuelimisha mazingira anayoishi ni mojawapo ya haki ya msingi.
Aidha ameeleza wajibu mwingine wa mzazi au mlezi kwa mtoto ni kumfundisha mtoto kazi za mikono,kwani wapo baadhi ya wazazi hawawafundishi watoto wao kazi za mikono jambo linalopelekea watoto kubweteka na kulemaa kiakili.
“Kuna wazazi wengine hawawafundishi wazazi kazi za mikono sasa hiyo ni moja ya sehemu ya kazi ya mzazi kumuelekeza mtoto afanye kazi za mikono na mfano mzuri hapa ni familia ya Yesu,Maria na Yoseph ambapo Yoseph alikuwa akimfundisha mtoto Yesu kazi za uselemala na Yesu akawa anazifanya.
Kwa hiyo sisi kama wazazi tunatakiwa kuwafundisha watoto wetu kazi mbalimbali za mikono ili waweze kuzijua kama ni kulima,kufagia,kuchota maji na shughuli zote zinazolingana na mazingira anayoishi mzazi.
Kwa hiyo mzazi ni lazima kumfundisha mtoto shughuli mbalimbali ili asibweteke kwa sababu maisha anayoishi asitegemee tu kwamba kutakuwa pengine kuna dada wa kazi ambaye atamfanyia kazi pasipo na yeye kufanya kazi.
Na akitegemea kufanyiwa kila kitu na Dada wa kazi atalemaa na kuona kwamba ni kawaida tu kufanyiwa kazi kumbe anajilemeza maisha yake yote na hayatakuwa mazuri,” alisema.
Hata hivyo Ndg Mhagwa aliwaomba wazazi na walezi wanapowalea watoto wao,wanapaswa kuangalia mazingira ya baadaye huku akiwataka kuwa waangalifu katika suala la teknolojia kwani lisipotumiwa vema linaweza kuharibu kizazi kilichopo na kijacho.
“Wajibu mwingine wa mzazi ni kumfundisha mtoto kutimiza madaraka yake mwenyewe.kwamba mtoto pengine inawezekana ndani ya familia ni Kaka au Dada lakini pengine anawaongoza wale wadogo zake au kaka zake kwa hiyo lazima atimize huo wajibu kama madaraka kwa maana ya kuwasimamia vema watoto ili waweze kutimiza wajibu wao.
Lakini wajibu mwingine wa mzazi ni kumfundisha mtoto kusema asante au kushukuru anapopewa kitu chochote kilicho chema manaake ni lazima ashukuru,kumfundisha kusema asante manaake ni sehemu tena ya kuongeza fursa ya kupata kingine.
Sasa mtoto anapokuwa anapewa kitu na hasemi asante manaake jamii inayomzunguka inamchukulia kwamba huyo mtoto hajafundishwa malezi mazuri kiasi cha kushindwa hata kusema asante.kwa hiyo kumfundisha mtoto kusema asante usisubiri tu hadi afikie umri flani ndo uanze kumfundisha,” alisema Ndg Mhagwa.
Alisema kwamba pamoja na wajibu na majukumu mbalimbali anayopaswa kufanya mzazi au mlezi kwa mtoto wake,kumfundisha Neno la Mungu ni moja ya wajibu mkubwa alionao mzazi au mlezi kwa mtoto.
Alisema Neno la Mungu kitabu cha Mithali 22:6 kinaeleza namna mzazi au mlezi anavyopaswa kumlea mtoto wake,ili njia zote anazopitia apite katika Neno la Mungu kwani maisha yote ya mwanadamu yamefumbatwa katika Neno la Mungu.
Aidha pamoja na wajibu huo wa kumfundisha Neno la Mungu,Ndg Mhagwa alisema kwamba wajibu mwingine wa mazazi ni kuzungumza bayana mambo yanayomhusu mtoto,ili kumjengea mtoto uhuru wa kuelezea yale anayokutana nayo.
“Yawezekana huko alikokuwa anacheza akaja kukwambia Baba au Mama kile alichokutana nacho kwa hiyo msikilize halafu uchukue hatua.kwa sababu sasa hivi watoto wanafanyiwa vitendo vya kikatili ikiwemo kulawitiwa na kubakwa sasa usipotenga muda wa kukaa na kumsikiliza mtoto ataendelewa kuathiliwa.kwa hiyo ni lazima tuzungumze na watoto tuone namna ya kuwasaidia,” alisema Ndg Mhagwa.
Sanjari na hayo alisema mzazi au mlezi anaowajibu wa kusikiliza kero na changamoto mbalimbali za mtoto.
“Wajibu mwingine wa mzazi au mlezi na kusikiliza kero za mtoto kwa sababu sasa hivi wazazi wana mambo mengi.mzazi anaondoka asubuhi anarudi jioni na akifika nyumbani amechoka na kuchoka kule anakosa muda wa kusikiliza kero za watoto.lakini mzazi unatakiwa kutega sikio lako usikilize kero za watoto,” alisema Ndg Mhagwa.