Featured Kitaifa

WAZIRI KIJAJI AFUNGUA JUKWAA LA PILI LA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA ITALIA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda
na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania inaendelea kuboresha
mazingira ya Uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ambapo tayari Mswada kuhusu
mapendekezo ya Sheria mpya ya Uwekezaji umesomwa bungeni hivi karibuni.

 

Mhe. Kijaji ametoa kauli
hiyo leo tarehe 30 Septemba 2022 wakati akifungua Jukwaa la Pili la Biashara na
Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika jijini Dar es Salaam na
kuwashirikisha wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na
Italia.

 

Mhe. Dkt. Kijaji ambaye alimwakilisha
Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye
ufunguzi wa Jukwaa hilo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais
Samia inaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya biashara na uwekezaji ili
kuwawezesha watanzania na wawekezaji kutoka nje kunufaika na fursa lukuki za biashara na
uwekezaji zilizopo nchini.

 

Amesema miongoni mwa
maboresho hayo ni mapendekezo ya Sheria Mpya ya Uwekezaji ambayo tayari
imesomwa Bungeni  hivi karibuni. Sheria
hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuwawezesha Watanzania wengi zaidi
kuwekeza kwenye miradi mikubwa ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa
ujumla.

 

Mhe. Dkt. Kijaji alitumia
fursa hiyo kuwaomba Watanzania na wadau mbalimbali wa uwekezaji kutoa maoni yao
kuhusu mapendekezo ya sheria hiyo ambayo tayari ipo wazi kwa umma wa watanzania
kwa ajili ya kutoa maoni yao.

 

“Watanzania wenzangu, tunapokutana
kwenye jukwaa hili la uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, Serikali yetu ipo
kwenye mchakato wa kuandaa Sheria mpya ya Uwekezaji na tayari tumeileta kwa
wananchi. Sheria hiyo inakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania,
ambapo pamoja na mambo mengine inapendekeza kushushwa kwa kiwango cha mwekezaji
mzawa kutoka mtaji wa Dola za Marekani 100,000 hadi 50,000.  Hivyo niwaombe watanzania wa kada zote,
wawekezaji, sekta binafsi ni wakati wetu sasa wa kutoa maoni yetu kuhusu sheria
hiyo” alisema Dkt. Kijaji.

 

Mhe. Kijaji ametaja
maboresho mengine yanayofanywa na Serikali kwenye Sekta ya Biashara na
uwekezaji kuwa ni pamoja na kuanzishwa mifumo ya kiteknolojia inayomrahisishia
mwekezaji namna ya kuanza biashara, kupata namba ya mlipa kodi, leseni, viza na
vibali vya kazi na ukaazi. Kadhalika serikali inakamilisha kuandaa mfumo wa
Kielektroniki kwa ajili ya kurahisisha utoaji mizigo bandarini.

 

Akizungumzia ushirikiano wa
kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, amesema unaendelea vizuri ambapo
hadi sasa Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimesajili miradi 111 kutoka Italia
yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 274.7 na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni
mwa wachangiaji wakubwa wa uwekezaji kutoka nje hapa nchini.

 

Pia amezitaka taasisi za
Serikali na Binafsi zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji hapa nchini kukutana
na kuandaa taarifa ya pamoja ikijumuisha changamoto na mafanikio yaliyoainishwa
wakati wa Jukwaa hili na kuzifanyia kazi changamoto hizo.

 

Akifunga Jukwaa hilo ambalo
limefanyika Zanzibar na Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amewapongeza waandaji wa Jukwaa hilo
wakiwemo Mabalozi wa Tanzania na Italia kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa
kupitia jukwaa hilo na kuahidi kuendeleza jukwaa hilo ili kufikia malengo
kusudiwa katika  utekelezaji wa diplomasia
ya uchumi.

 

“Nawapongeza waandaji wa
Jukwaa hili muhimu wakiwemo Mabalozi wetu  na sitalifunga bali nitaliahirisha
ili wakati mwingine tuendelee pale tulipoishia” alisema Balozi Mulamula.

 

Kwa upande wake, Balozi wa
Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ameendelea kutoa wito kwa
watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za masoko kama matunda, maua nchini
Italia ili kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia katika kukuza uchumi wa nchi.

 

Naye Balozi wa Italia hapa
nchini amesisitiza kuendelea kutoa ushirikiano wowote unaohitajika ili kuimarisha
ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kupitia majukwaa mbalimbali ya ushirikiano.

 

Jukwaa la Pili la Biashara
na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limefanyika Zanzibar na Dar es Salaam
kuanzia tarehe 27 hadi 30 Septemba 2022. Jukwaa hili limewakutanisha wawekezaji
na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia.   

 

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kikaji akifungua kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba 2022.

 

Sehemu ya wageni waalikwa wakiwemo wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia wakifuatilia hotuba ya ufunguzi

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akihutubia wakati wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia

 

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombp akizungumza wakati wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia

 

Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi nae akizungumza wakati wa Jukwaa hilo

 

Sehemu nyingine  ya washiriki wakiwa kwenye mkutano
Sehemu nyingine ya Washiriki wakati wa mkutano wa Jukwaa hilo
Mhe. Dkt. Kijaji akiwa katika picha ya pamoja na washiriki

 

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki

 

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Kombo (kulia), Balozi wa Italia nchini, Mhe. Lombardi (kushoto) na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania jijini Milan, Italia, Bw. Cecil

 

Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania, Italia na Balozi wa Italia nchini pamoja na Mabalozi wastaafu, Balozi Modest Mero (kulia aliyesimama) na Balozi James Msekela (kushoto)


About the author

mzalendoeditor