Featured Kitaifa

“USHURU WA HUDUMA KWA WANANCHI NA WAFANYA BIASHARA NI KUSAIDIA HALMASHAURI”-THERESIA COSMAS

Written by mzalendoeditor

MHASIBU wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Theresia Cosmass aeleza faida za ushuru wa huduma kwa wananchi na wafanyabiashara kuwa ni kusaidia Halmashauri kupata mapato yatakayotekeleza miradi ya kimaendeleo na kuimarisha huduma za kijamii.

Alisema hayo alipokuwa katika oparesheni ya kukusanya mapato katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kata ya Ihumwa Mtaa wa Flamingo, ikiwa ni siku ya pili ya oparesheni hiyo.

Cosmass alisema kuwa ushuru wa huduma ni muhimu kwani hupelekea maboresho ya miundombinu na kuimarisha huduma za kijamii ambapo itasaidia wananchi kupata huduma nzuri na kwa urahisi.

“kodi ya ushuru wa huduma itasaidia kuboresha huduma za kijamii kama hospitali, ujenzi wa barabara na kwa wafanyabiashara miundombinu ya barabara ambayo itasaidia biashara zao kufikika kwa urahisi” alisema Cosmass.

Naye Afisa Biashara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Amri Kibwana aliongeza kuwa mwitikio wa operesheni hiyo ni chanya na wafanyabiashra wanachukua hatua kama inavyoelekeza sheria baada ya kupatiwa elimu.

“Pale tunapokuta mapungufu, tunatoa elimu na kuwapa maelekezo namna ya kuanza mchakato wa kulipa ushuru wa huduma na wafanyabiashara wanamwitikio mzuri wanakuja ofisini kwaajili ya kufanya malipo” alisema Kibwana.

Akitoa wito kwa wafanyabiashara wengine, Sospeter Kanichi amabae ni mfanyabiashara wa bucha ya nyama alisema kuwa wafanyabiashara wafuate maelekezo kwa kulipa ushuru wa huduma kwasababu ni njia majawapo ya kuchangia maendeleo ya nchi.

“Ni sahihi kulipa ushuru wa huduma kwasababu tunachangia serikali yetu na tunaboresha nchi yetu lakini pia biashara zetu. Hivyo, watu wasikimbie” alisema Kanichi.

Oparesheni hiyo iliyoanza jana itadumu kwa siku tatu na baadae itafanyika oparesheni kwaajili ya kukagua utekelezaji.

About the author

mzalendoeditor