Featured Kitaifa

MAKAMU WA RAIS: SERIKALI INATHAMINI MCHANGO WA MADHEHEBU YOTE YA DINI

Written by mzalendoeditor
Imeelezwa kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa Madhehebu ya dini kupitia mahubiri na kufundisha neno la Mungu kwa watu wote.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko katika Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 75 ya Kanisa la Elimu Pentekoste Tanzania (KEPT) iliyofanyika Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Dkt. Biteko ametoa pongezi kwa niaba ya Serikali kwa mambo yanayofanyika ya kuhuburi kwa watu na Taifa kwa ujumla ikiwemo kufundisha neno la Mungu kwa watu wote.
Pia, amewapongeza kwa kutoa huduma za kijamii ikiwemo elimu na afya, kuendelea kuhimiza waumini wote kudumisha amani, upendo, mshikamano na utulivu kwa kufanya kazi kwa bidii pamoja na kutunza mazingira.
Dkt.Biteko amesema, Mhe. Rais Samia ameendelea kusisitiza kuwahudumia watanzania kwa heshima kubwa ili maisha yao yazidi kuwa bora kila wakati.
“Nitoe mfano kwa sekta ninayoiongoza ya Madini, tangu Mhe.Rais ameingia madarakani ametuelekeza kufuta baadhi ya kodi mbalimbali ambazo wachimbaji wadogo walikuwa wanaona ni kero katika shughuli zao.
Pia, Mhe. Rais amesisitiza kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji wa ndani na nje kwa kufuta baadhi ya vipengele vya Sheria na Kanuni ambavyo vilikuwa vinakwaza uwekezaji.
“Yote haya, Mhe. Rais anayafanya kwa sababu kiu yake ya kuona kila mwananchi ndani ya nchi hii anakuwa na furaha na maisha yake, na kufurahia kufanya kazi anayoifanya kwa ajili ya kuendeshea maisha yake,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko kwa niaba ya Makamu wa Rais ameshiriki katika uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa jengo la kanisa na upandaji wa mti wa kumbukumbu.
Kwa upande wake, Baba Askofu Mkuu wa KEPT, Peter Konki amesema, kanisa lilianzishwa na Wamisionari kutoka Uingereza mwaka 1946 nchini Tanzania.
Amesema, walifungua makanisa ya kwanza wilaya ya Kondoa mkoa wa Dodoma, Msolwa katika mkoa wa Pwani, Tanga na wilaya ya Babati Mkoani Manyara.
Askofu Konki ametoa wito kwa jamii na watanzania kushiriki katika kudumisha amani na utulivu iliyopo kwa vitendo na kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuishi maisha mema.
Hafla ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 75 ya KEPT imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Babati, Pauline Gekul, Maaskofu Wakuu kutoka Madhehebu mengine na waumini mbalimbali.

About the author

mzalendoeditor