Featured Kitaifa

GGML,RC GEITA WAZINDUA MPANGO WA UPANDAJI MITI

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella (kulia) akipanda mti pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited, Terry Strong mwishoni mwa wiki pembezoni mwa Barabara ya Nyerere mjini Geita katika uzinduzi wa kampeni ya kuifanya Geita kuwa ya kijani.

……………………………………………..

NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita na Halmashauri ya Mji wa Geita imezindua mpango wa upandaji miti katika mji wa Geita na kando ya Barabara ya Geita-Mwanza kwa lengo la kuupendezesha na kuufanya mji huo kuwa wa kijani.

Akizungumza katika hafla hiyo kwenye eneo la Bombambili mjini Geita juzi Mjini Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella alitoa wito kwa jamii ya Geita kujenga hulka ya kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuifanya Geita kuwa ya kijani.

“Naipongeza kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), taasisi za ulinzi na usalama na viongozi wa serikali waliokusanyika hapa kutuunga mkono katika mpango huu. Tumekubaliana kutekeleza zoezi hili kila mwezi ili kufikia malengo ya kupanda miti katika maeneo mengi zaidi. Tungependa kuona Geita ikibadilika kuwa kijani kwa kuwa na bustani na miti ya kisasa na iliyotunzwa vizuri.

“Leo tumetembea kilometa tatu na kupanda miti mingi lakini mwezi ujao, tutaenda mbali zaidi kuelekea eneo la Magogo ilipo ofisi yangu na ya Halmashauri ya Mji wa Geita,” alisema Mkuu huyo wa mkoa.

Akizungumza kwa upande wa GGML, Mkurugenzi Mtendaji, Terry Strong alieleza kufurahia kuwa sehemu ya mpango huo na kuipongeza ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuja na mpango huo muhimu ambao umekuja wakati muafaka katika kipindi cha msimu wa mvua.

“Naipongeza ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Mkurugenzi wa Mji kwa kuja na mpango huu. AngloGold Ashanti – Geita Gold Mining Limited, tumedhamiria kuhifadhi na kuboresha mazingira kwani hii ni moja ya tunu zetu za msingi,” alisema.

Aliongeza kuwa GGML imekuwa ikiendesha kampeni kadhaa za mazingira tangu mwaka 2000 ilipoanza shughuli zake za uchimbaji mkoani Geita.

“Ni vyema kutambua kuwa zaidi ya asilimia 70 ya leseni yetu maalum ya uchimbaji madini ipo ndani ya hifadhi ya msitu wa Geita ambayo inahitaji kupandwa miti mara kwa mara ili kuilinda na kwa maendeleo endelevu ya Tanzania  na manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

“Nina matumaini yangu kuwa kupitia shughuli hizo, jamii itaelewa athari za uhifadhi wa mazingira na kuondokana na vitendo vya ukataji miti ambavyo vina madhara makubwa katika maisha yetu ya kila siku,” aliongeza Terry Strong.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella (kulia) akipanda mti pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited, Terry Strong mwishoni mwa wiki pembezoni mwa Barabara ya Nyerere mjini Geita katika uzinduzi wa kampeni ya kuifanya Geita kuwa ya kijani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited, Terry Strong akizungumza na waandishi wa habari namna kampuni hiyo inavyoungana na Serikali kulinda na kuhifadhi mazingira.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella (wa kwanza kulia) akizungumza na wageni waalikwa (hawapo pichani) waliohudhuria halfa ya uzinduzi wa mpango wa mkoa huo kupanda miti na kuifanya Geita kuwa ya kijani. Watatu kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited, Terry Strong ambaye kwa pamoja mwishoni mwa wiki walishiriki kupanda miti pembezoni mwa Barabara ya Nyerere mjini Geita.

About the author

mzalendoeditor