Askofu Mkuu wa Kanisa la Hebrews Camp Church For All Nations Lameck Kasumba Maguluchini amesema yuko tayari kutumika shambani mwa Bwana baada ya kusimikwa kuwa Askofu Mkuu Jumapili 11 Septemba 2022.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusimikwa rasmi, Askofu Mkuu Lameck Kasumba Maguluchini amesema kazi ya Mungu inahitaji watu walio tayari na yeye ni mmoja wa watumishi walio tayari kumtumikia Mungu kwa ukubwa zaidi.
“Namshukuru Mungu kwa kwa hatua hii ya kusimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Hebrews Camp Church For All Nations. Nimekuwa nachunga Kondoo wa Bwana kwa muda wa kutosha, Mungu ameona nipate hatua hii ya kuwa Askofu Mkuu, ninamshukuru Mungu sana.” alisema Askofu Mkuu Lameck Kasumba Maguluchini.
Aidha Askofu Maguluchini ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kulipa kanisa hilo usajili wa kufanya huduma zake za kiroho nchini Tanzania. Amesema hatua hiyo kubwa kwa kutambuliwa na Serikali ya Tanzania.
Akihubiri Kanisani hapo kabla ya kumsimika Mchungaji Lameck Kasumba Maguluchini kuwa Askofu, Askofu Mkuu wa kanisa la CECT Dr Charles Sekelwa alisema amemfahamu kwa muda mrefu Askofu Lameck, amekuwa mlezi wake kiroho na anajua anao uwezo mkubwa wa kuwa Askofu Mkuu.
“Askofu Lameck amekuwa mwanangu niliyemlea kiroho miaka sita sasa, ninajua uwezo wake wa kusimamia kazi ya Mungu. Ninaamini atafanya vizuri katika nafasi hii, na leo nimemsikimika rasmi kuwa Askofu Mkuu” alisema Askofu Dr Charles Sekelwa.
Katika halfa hiyo ambayo ilifanyika katika viwanja vya kanisa la HCCFAN lililopo Nyahingi Mkolani wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo kutoka Serikali ya Mkoa wa Mwanza, wilaya ya Nyamagana, viongozi wa madhehebu mbalimbali pamoja na waumini kutoka maeneo tofauti tofauti nchini Tanzania.
Huduma ya Hebrews Camp Church For All Nations ina waumini zaidi ya elfu mbili kutoka katika parish kumi na tatu zilizopo Tanzania na makao makuu ya huduma yanapatikana Nyahingi Mkolani Nyamagana Mwanza.