Na Tamimu Adam – Jeshi la Polisi.
WANANCHI wametakiwa kujitokeza katika kampeni maalum ya mwezi wa msamaha wa Afrika itakayohusisha usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari katika vituo vya polisi, ofisi za Serikali za mitaa, ofisi za watendaji wa Serikali za mitaa na vijiji.
Rai hiyo imetolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Kampeni maalumu ya Usalimishaji wa silaha itakayozinduliwa Septemba 5, 2022 katika viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma.
Misime alisema kuwa kampeni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mhandisi Hamad Yusuph Msauni na itaendelea kuzinduliwa katika mikoa mbalimbali nchini ili taarifa ziweze kuwafikia wananchi wote.
Aliwataka wananchi wa mkoa Dodoma na mikoa mingine kuhudhulia uzinduzi huo ili waweze kupata elimu na uelewa juu ya madhara ya kumiliki silaha kinyume na sheria pamoja na kujua utaratibu wa kisheria kumiliki silaha.
Uzinduzi huo utapambwa na burudani mbalimbali kutoka bendi ya shule ya Polisi Tanzania (Super Kwata bend ) pamoja na Msanii wa Polisi, kutoka kamisheni ya Polisi Jamii Staff Sajenti Malima Mjinja anayejulikana kwa jina la kisanii Ndolera