Featured Kitaifa

WAZIRI MWIGULU ATOA UFAFANUZI WA AWALI MALALAMIKO YA MIAMALA YA SIMU NA BENKI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Septemba 1,2022 jijini Dodoma kuhusu ufafanuzi wa masuala ya tozo kwenye miamala ya Simu na benki.

………………………………..

Na.Eva Godwin-DODOMA

SERIKALI  imetolea ufafanuzi wa awali suala la tozo kwenye miamala ya kibenki na kubainisha kuwa imeweka tozo kwenye miamala ya benki lengo ni kupunguza mzigo wa tozo kwenye miamala ya simu.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 1,2022 jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya malalamiko ya wananchi kwenye tozo ambapo amesema wameongeza wigo wa tozo ili kufikisha huduma stahiki za kijamii kwa wananchi.

Amesema tozo kwenye miamala ya simu zimeshuka kutoka shilingi elfu saba hadi elfu nne kwa kiwango cha juu.

 ”Serikali imewataka Wananchi kuwa watulivu juu ya suala la tozo huku ikiwawashukuru wananchi hao kwa kutoa maoni yao ya suala hilo la tozo na kwamba imewasikia, imepokea hivyo hivi karibuni itakuja na majibu sahihi.”amesema Dk.Nchemba

Dk. Mwigulu amesema serikali imeweka timu ya watu kwa ajili ya kuchambua tozo hizo kwani ni lazima mtu alipe kulingana na kipato chake na sio kuwaonea wanyone huku wenye uwezo mkubwa wa kipato wakiachwa.

“Hii Nchi yetu sote na hii Nchi ni yawatanzania Kila mtanzania anayohaki ya kutoa maoni na sisi kama Serikali tunayachukia na kuyafanyia kazi,maoni ya wananchi ni muhimu sana kwetu na ndio maana tunayapokea”amesema

Serikali ipo kwaajili ya kupokea maoni ya wananchi inahakikisha inayapokea na kuyafanyia kazi muda wote hakuna Serikali bila wananchi,Tanzania inajengwa na watanzania wote,”amesema Dkt.Mwigulu.

Waziri Nchemba amebainisha kuwa katika nchi za Afrika Mashariki na za Jumuiya ya Kiuchumi nchi za kusini mwa Afrika (SADC), hakuna nchi inyotekeleza kwa mara moja miradi mikubwa kama Tanzania.

Waziri huyo ameeleza kuwa Tanzania ina bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo ni la lazima nchi inalihitaji tangu siku nyingi, bajeti yake ni zaidi ya Trilioni 6, Reli ya kisasa hadi kukamilika inahitaji zaidi ya trilioni 23.

“Kila Mtanzania anatakiwa ajisikie farahi kwa miradi mikubwa ambayo ni uti wa mgongo ambayo itageuza uchumi wa chi yetu, Chimbuko la tozo ilikuwa ni kwa ajili ya kuunganisha nguvu kama Watanzania ili tuweze kutekeleza mahitaji ya lazima ambayo yalikuwa pengine yanakosa bajeti. ,”amesema Waziri Mwigulu.

Katika hatua nyingine Dkt. Mwigulu,ametolea  ufafanuzi suala la kodi za majengo  huku akibainisha kuwa wanaangalia namna bora ya ukusanyaji wa kodi hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 Serikali ilitoa Shilingi bilioni 117 za Tozo za Miamala ya Simu kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 234 kwenye Tarafa na Kata ambazo hazikuwa na Vituo vya Afya.

Amesema kuwa ujenzi wa kila Kituo cha Afya umegharimu Shilingi milioni 500 na umefanyika kwa upelekaji wa fedha kwa awamu 2, ambapo awamu ya kwanza zilipelekwa Shiilingi milioni 250 na baadae Shilingi milioni 250 kukamilisha.

”Haijapata kutokea tangu tupate uhuru, kujengwa Vituo 234 kwa wakati mmoja ndani ya mwaka mmoja wa fedha ambapo Ujenzi ulihusisha majengo ya Wagonjwa wa Nje (OPD), Maabara, Jengo la Wodi ya Wazazi, Jengo la Upasuaji na Jengo kwa ajili ya Kufulia” amesema Bashungwa.

Aidha  Waziri Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa miradi ambayo ilipokea fedha mwishoni mwa mwaka wa fedha 2021/22 na ikamilike kwa wakati ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi ndani ya miezi minne baada ya kupokea fedha za ujenzi.

Naye  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,kazi,vijana,Ajira na wenye ulemavu Prof.Joyce Ndalichako alisema kuwa chini ya uongozi wa awamu ya 6 ni elimu bila malipo kuanzia awali mpaka kidato Cha sita.

Pia amewahahkikishia wafanyakazi kutokuwa na mashaka na uwakikishi wa viongozi wa vyama vyao.

Amesema kilio kikubwa Cha wafanyakazi ilikuwa ni lazima mishahara ipite banki na wanapotaka kutoa fedha kwenda kwenye simu pia makato yanakuwepo ikiwa wafanyakazi hao hawalidhishwi na utaratibu huo.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Septemba 1,2022 jijini Dodoma kuhusu ufafanuzi wa masuala ya tozo kwenye miamala ya Simu na benki.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa,akizungumza  katika mkutano na vyombo vya habari kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala ya tozo kwenye miamala ya Simu na benki ulioandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango uliofanyika leo Septemba 1,2022 jijini Dodoma.

Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu George simbachawane,akizungumza  katika mkutano na vyombo vya habari kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala ya tozo kwenye miamala ya Simu na benki ulioandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango uliofanyika leo Septemba 1,2022 jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ,akizungumza  katika mkutano na vyombo vya habari kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala ya tozo kwenye miamala ya Simu na benki ulioandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango uliofanyika leo Septemba 1,2022 jijini Dodoma.

About the author

mzalendoeditor