Featured Kitaifa

WAZIRI UMMY AELEZA CHANZO CHA MFUKO WA BIMA YA AFYA KUELEMEWA

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu hali ya mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Leo 1 Septemba, 2022 Jijini Dodoma.

……………………………………

Na Eva Godwin-DODOMA
WIZARA ya Afya imeeleza chanzo ya kuelemewa kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF),kuwa ni kuongezeka kwa idadi kubwa ya wananchi wenye magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ambayo gharama zake ni kubwa.

Ameyasema hayo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu hali ya mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambapo hatua hiyo imekuja baada ya kuibuka kwa sintofahamu hivi karibuni kuhusu mfuko huo, leo 1 Septemba 2022 Jijini Dodoma.

Amesema kuwa Agosti 29 mwaka huu wakati akifungua Mkutano wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika kuhusu Ugonjwa wa Kipindupindu Jijini Dar es Salaam,aliweka msisitizo wa kuweka nguvu na jitihada katika kuzuia magonjwa badala ya kusubiri kutibu.

“Katika muktadha huo nilitoa angalizo kuwa hivi sasa nchini kwetu tunashudia ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo matibabu yake ni gharama kubwa na hivyo kama tutachelewa kuchukua hatua stahiki katika kudhibiti magonjwa hayo, basi kuna hatari pia kwa Mfuko wetu wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuelemewa na gharama za matibabu

“Na hii inatokana na kuongezeka kwa idadi ya wanufaikaji wenye magonjwa yasiyoambukizwa na gharama zake, hali inayoweza kuathiri uhai na uendelevu wa Mfuko”. Amesema Ummy

Amesema kulingana na takwimu zilizopo, gharama za magonjwa yasiyo ya kuambukizwa zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 35.65 mwaka 2016/17 hadi shilingi bilioni 99.09 mwaka 2021/22,
Huku gharama za kuhudumia wagonjwa wa saratani wanaopata tiba za mionzi na chemotherapia (chemotherapy services), kupitia Mfuko ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 22.5 mwaka 2021/22.

“Kwa upande wa huduma za matibabu ya figo kwa wanachama wanaopata huduma ya kuchuja damu (hemodialysis services), gharama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9.5 mwaka 2015/16 kufikia shilingi bilioni 35.44 mwaka 2021/22, na idadi ya wagonjwa hawa wa figo imeongezeka kutoka 280 mwaka 2014/15 hadi kufikia 2,099 mwaka 2021/22”, amesema

“Ambapo gharama za matibabu ya moyo kwa wanachama wa Mfuko wanaopata matibabu ya upasuaji wa moyo (minimal and invasive cardiac procedures), ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 0.5 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 4.33 mwaka 2021/22”, amesema

Ameongezea kuwa Gharama za vipimo vya CT scan na MRI ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 5.43 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 10.87 mwaka 2021/22.

“Kwa muelekeo wa takwimu hizi, ni wazi kuwa kama hatutachukua hatua madhubuti kama nchi, kuna uwezekano wa Mfuko kwa siku za mbeleni kushindwa kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria”, amesema

“Hatua hizo zinaanzia katika ngazi ya mtu mmoja mmoja kwa kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia aina za vyakula tunavyokula, kuepuka uvutaji wa sigara na kufanya mazoezi hata hivyo Serikali kuendelea kubuni mikakati ya kukinga magonjwa haya na pia kupambana nayo kadri yanavyojitokeza”. Amesema Ummy

Kutokana na hayo Waziri Ummy aliielekeza NHIF kuimarisha mikakati yake ya kupambana na vitendo vya udanganyifu pamoja na kuimarisha matumizi ya Mifumo ya TEHAMA,
na pia alitaja changamoto nyingine iliyopo ni uwepo wa kundi kubwa la wananchi wanaojiunga na NHIF kwa hiari ambao, takribani asilimia 99 ni wagonjwa.

“Hatua hii imetokana na kutokuwepo kwa Sheria ya ulazima kwa wananchi kujiunga na Bima ya Afya,kama mnavyokumbuka (NHIF)ulianzishwa mwaka 2001 ukiwa umelenga kuwahudumia watumishi wa umma pekee.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu hali ya mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Leo 1 Septemba, 2022 Jijini Dodoma.

About the author

mzalendoeditor