Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na Rais wa Tunisia Kais Saied alipowasili katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres kuhudhuria Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8), mjini Tunis,Tunisia, Agosti 27, 2022. Waziri Mkuu anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemshukuru Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida kwa misaada ambayo nchi yake inaipatia Tanzania ili kuleta unafuu kwenye maisha ya wananchi wake.
“Tanzania tunaishukuru sana Serikali ya Japan kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwakwamua wananchi wake kiuchumi na kuwezesha ujenzi wa miundombinu hadi vijijini,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Agosti 27, 2022) wakati akizungumza naye kwa njia ya mitandao kwenye ukumbi wa Palais des Congres, jijini Tunis, Tunisia. Mheshimiwa Kishida ameshindwa kuhudhuria mkutano kwa sababu ya maambukizi ya UVIKO 19.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye anamwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa TICAD ulioanza leo, alimweleza Waziri Mkuu huyo kwamba Tanzania bado inaomboleza na wananchi wa Japan kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Shinzo Abe na akatumia fursa hiyo kuwapa pole.
Akigusia miradi ambayo Serikali imeisaidia Tanzania, Waziri Mkuu amesema: “Iko miradi mingi ambayo imetekelezwa na Japan kupitia taasisi ya JICA, wako wawekezaji wanafanya biashara nasi na pia yako makampuni ambayo yamejitoa kusaidia sekta muhimu.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuiomba Japan ikamilishe ahadi yake ya kutekelza miradi waliyoiahidi kwenye mkutano wa TICAD 7 ambayo inahusu ujenzi wa barabara ya Arusha mpaka Holili mkoani Kilimanjaro, mradi wa maji wa Zanzibar, ujenzi wa bandari ya Kigoma na bandari ya uvuvi Zanzibar.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan, amemtumia salamu Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote na akataka uhusiano wa nchi hizo mbili kupitia taasisi yao ya JICA.
Mapema, akitoa tamko kwa niaba ya Rais Samia kwenye mkutano huo wa wakuu wa nchi na Serikali, Waziri Mkuu alisema bara la Afrika linakabiliwa na matatizo ya kiuchumi ambayo kwa kiasi kikubwa chimbuk lake ni UVIKO 19.
“Nimewaeleza madhara ya UVIKO 19 ambayo yanaikumba Afrika Tanzania ikiwemo, matatizo ya vita ya Ukraine na Urusi ambavyo vimesaabisha bei za bidhaa nyingi kupanda. Nimewaambia ujko umuhimu wa mataifa makubwa ya G20 kuungana na Japan ambayo ni ya tatu kwa ukubwa kiuchumi ili kuzisaidia nchi za Afrika.”
Amesema iko haja ya kuziwezesha nchi za Afrika kujitegemea ili ziweze kuwasaidia wananchi wake kupata fursa za elimu, kujenga uweza wa shughuli za kilimo, utalii ili waweze kukuza uchumi wao.
Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Rais Tunisia, Mhe. Kais Saied ambapo Rais wa Senegal, Mhe. Macky Sall alitoa hotuba ya ufunguzi na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Kishida Fumio akahutubia kwa njia ya mitandao kutokea Japan.
Pamoja na masuala mengine, mkutano huo wa siku unatarajiwa kukubaliana kuhusu namna ya kuiwezesha Afrika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Dunia ili kuiwezesha kufikia Agenda ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (Agenda 2063).
Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na janga la UVIKO 19, amani na usalama, mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji mgumu wa malighafi na mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazotegemewa na nchi za Afrika kama vile gesi, mafuta na pembejeo za kilimo ambazo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Bara la Afrika.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akifuatilia Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) unaoendelea katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres mjini Tunis,Tunisia, Agosti 27, 2022. Waziri Mkuu anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Tunisia Kais Saied alipowasili katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres kuhudhuria Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8), mjini Tunis,Tunisia, Agosti 27, 2022. Waziri Mkuu anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo.