Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU AWASILI TUNISIA KUHUDHURIA MKUTANO WA TICAD

Written by mzalendoeditor

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasili Tunisia leo (Ijumaa Agosti 26, 2022) na kupokelewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mhe. Najla Bouden Romdhane katika uwanja wa ndege wa Carthage, jijini Tunis.

Waziri Mkuu anatarajiwa kumwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa TICAD ambao unaanza kesho Jumamosi, Agosti 27, 2022.

Katika mazungumzo yao uwanjani hapo, Waziri Mkuu alipata wasaa wa kubadilishana mawazo na mwenyeji wake ambapo walijadiliana masuala kadhaa kuhusu demokrasia na utawala bora, uhusiano wa kimataifa na uchumi.

Mkutano huo utakaofanyika Agosti 27-28, 2022 unatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano na ajenda za kimaendeleo zitakazotekelezwa kati ya Japan na Afrika. Rais wa Senegal, Mhe. Macky Sall na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Kishida Fumio watatoa hotuba za ufunguzi wa mkutano huo.

Tanzania imekuwa ikishiriki mikutano hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993. Kufuatia mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Japan hususani kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), Tanzania imekuwa ikinufaika na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za miundombinu ya barabara, nishati ya umeme, maji, elimu, afya na kilimo.

About the author

mzalendoeditor