Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na viongozi wa Wilaya ya Kinondoni kwenye kikao alichokiitisha Ofisini kwake Oysterbay, Dar es Salaam.
……………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka mitatu katika eneo la Boko-Dovya, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam baina ya Bw. Aloyce Mwasuka na Bw. Salutari Massawe.
Katika mgogoro huo unaohusisha viwanja namba 393, 395 na 370 kwenye kitalu G (Boko Dovya) vilivyoko njiapanda ya Mbweni, Bw. Massawe alijenga ukuta ambao ulikuwa unazuia matumizi ya barabara na hivyo kumfanya Bw. Mwasuka apitie kwa jirani yake Bi. Oliver Semuguruka (kiwanja na. 395) ili aweze kufika nyumbani kwake (kiwanja na. 393).
Akizungumza na watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, watendaji wa Wilaya ya Kinondoni katika kikao alichokiitisha leo (Jumatano, Agosti 17, 2022) ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na hatua aliyoichukua Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Godwin Gondwe ya kusimamia uvunjaji wa ukuta huo ili kupisha eneo la barabara.
“Ninakushukuru Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na timu yako kwa kuchukua hatua tangu jana ili kusimamia haki ya wananchi wasio na uwezo. Haki ni ya kila mmoja, mwenye uwezo na asiye na uwezo. Ile barabara iboreshwe ili wananchi wote wanufaike,” amesema.
Waziri Mkuu amesema hatua hiyo inaenda sambamba na utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyowapa wasaidizi wake akitaka wahakikishe kuwa wananchi hawapati shida kwenye maeneo yao.
Akisisitiza usimamizi wa majukumu yao kwa watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri Mkuu amesema: “Nendeni mkasimamie masuala ya ardhi ili Watendaji wa Serikali nao wafanye kazi nyingine za kuwahudumia wananchi. Lazima tufanye mifumo isimamiwe ili kazi nyingine ziendelee,” amesisitiza.
Mapema, akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni alisema eneo hilo limeainishwa kwenye ramani ya mipango miji ya mwaka 2002 (TP 2002) na kwamba Bw. Massawe alinunua eneo hilo mwaka 2004 na akalipima mwaka 2005, wakati Bw. Mwasuka alinunua eneo lake mwaka 2005 na akalipima mwaka 2006.
“Katika upimaji wao kila mmoja alitumia mpimaji wake lakini coordinates zinaonesha kuwa kuna barabara katikati yao na ramani zao pia zinatambua barabara hiyo. Wote wawili walipaswa kuheshimu michoro ya mipango miji ambayo ni michoro mama,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Naye Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Idrissa Kayera alimweleza Waziri Mkuu kwamba licha ya kuwa ramani zote mbili zimeitambua barabara hiyo yenye upana wa mita 12, Bw. Massawe aliamua kujenga ukuta upande mmoja tu katika eneo lake ambao uliziba eneo hilo la barabara na hivyo kufunga barabara inayotenganisha viwanja namba 393, 395, 370, 391,390 na 369.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Ridhiwan Kikwete alisema Wizara itaendelea kusimamia migogoro yote iliyopo na kuweka mpango wa kuishughulikia.
Bw. Aloyce Mwasuka alimshukuru Waziri Mkuu, Naibu Waziri, Mkuu wa Wilaya na timu yao ya watendaji kwa kutatua migogoro huo na akaomba timu hizo mbili ziendelee kushirikiana ili kuwasaidia wananchi wengine wasio na sauti. Bw. Massawe hakufika kwenye kikao hicho kwa sababu ya changamoto ya kiafya.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na viongozi wa Wilaya ya Kinondoni kwenye kikao alichokiitisha Ofisini kwake Oysterbay, Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete kuhusu ramani ya eneo lenye mgogoro lililoko Boko – Dovya, wilayani Kinondoni katika kikao alichokiitisha ofisini kwake Oysterbay, Dar es Salaam, Agosti 17, 2022. Mgogoro huo umedumu kwa miaka mitatu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)