Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA VIFO VYA WATU 19 KWA AJALI MKOANI MBEYA

Written by mzalendoeditor

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera kufuatia vifo vya watu 19 vilivyotokea katika ajali ya gari.

Ajali hiyo imetokea leo saa mbili asubuhi katika eneo la Shamwengo kata ya Inyala tarafa ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Ulrich Matei, waliopoteza maisha ni watu 19 (wanawake 6, wanaume 12 na mtoto 1) na majeruhi ni 25.

SACP Matei amesema ajali hiyo imehusisha lori lililokuwa likitoka Mbeya kwenda Dar es Salaam, lenye namba za usajili T387 DSJ na tela namba T 918 DFE mali ya Kampuni ya Everest French Limited.

Lori hilo iliyokuwa imebeba kontena la mchanga ililigonga kwa nyuma basi la abiria la Kampuni ya Super Rojas iliyokuwa ikitoka Mbeya kwenda Njombe.

Aidha, basi hilo nalo lililigonga kwa nyuma gari ndogo aina ya Benz yenye namba ya usajili T 836 DRE ambalo nalo liligonga Lori lililokuwa limebeba kontena lenye namba ya usajili T342 CHG na tela namba CGS kwa nyuma.

Rais Samia anawapa pole majeruhi wa ajali hiyo pamoja na wafiwa wote pia anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema Peponi. Amina.

Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

About the author

mzalendoeditor