Featured Kitaifa

BARABARA YA SAADANI HADI TANGA KUCHOCHEA USAFIRISHAJI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Tanga, Eng. Eliazary Rweikiza, wakati akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange (km 95.2), ikiwemo na kilometa 3.7 za mchepuo wa barabara ya Kipumbwi kwa kiwango cha lami, mkoani Tanga.

……………………………….

Imeelezwa kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange (km 95.2), ikiwemo na kilometa 3.7 za mchepuo wa barabara ya Kipumbwi inayojengwa kwa kiwango cha lami itafungua fursa za usafiri na usafirishaji katika mwambao wa Tanga na mikoa ya jirani.

Hayo yamesemwa mkoani Tanga na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alipoutembelea na kuukagua mradi huo unaogharimu takriban ya shilingi Bilioni 94.53 ambao umeanza mwezi Aprili, 2022.

“Mradi huu ni mradi wa pamoja kati ya nchi yetu na nchi ya Kenya ambayo itamruhusu msafirishaji kutoka kuanzia Bagamoyo – Saadani – Tanga – Horohoro/Lunga lunga nchini Kenya – Mombasa mpaka Lamu kupitia barabara hii ambapo na wenzetu wanaendelea na ujenzi wa barabara hii kwa sehemu yao”, amefafanua Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa barabara hiyo itafungua fursa nyingi ikiwemo Sekta ya Utalii kwani itawezesha watalii kutoka nchi za jirani na kuja kutembelea hifadhi ya Saadani na visiwa vya Zanzibar kwa urahisi.

Aidha, amemtaka mkandarasi kujipanga vyema katika mpango kazi wake ili kukamilisha mradi huo ambao unasubiri kwa hamu kubwa na wananchi wa mikoa ya Pwani na Tanga kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kiuchumi.

Kuhusu fidia za wananchi waliopisha mradi huo, Waziri Mbarawa ameutaka Wakala wa Barabara (TANROADS), kuhakikisha wanatoa elimu kwa baadhi ya wananchi ambao wanakuwa na ukakasi wa kupisha maeneo ya miradi inayoendelea kutekelezwa hapa nchini na hivyo kupelekea miradi ya miundombinu kutokukamilika kwa wakati.

“Nichukue fursa hii kwa watanzania wenzangu waliopitiwa na mradi huu waruhusu ujenzi uendelee na mkandarasi afanye kazi yake kama wana malalamiko waje Wizara kwa utaratibu na watasikilizwa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Tanga, Eng. Eliazary Rweikiza ameeleza kuwa hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 6.23 ambapo kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa kambi ya mkandarasi umekamilika kwa asilimia 100 na kambi ya Mhandisi Mshauri imefikia asilimia 75.

Eng. Rweikiza ameongeza kuwa kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na kusafisha barabara, uchimbaji wa udongo, kuweka tabaka la kifusi na kuendelea kutengeneza makalvati ya zege katika barabara hiyo.

Ujenzi wa barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange (km 95.2), ikiwemo na kilometa 3.7 za mchepuo wa barabara ya Kipumbwi  kwa kiwango cha lami unatekelezwa na muda wa miezi 36 na mkandarasi China Railway 15 Burea Group Corporation na kusimamiwa na Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya  Beza Consulting Engineering  kwa kushirikiana na Chiel Engineering na Afrisa Consulting wa Ethiopia.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Tanga, Eng. Eliazary Rweikiza, wakati akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange (km 95.2), ikiwemo na kilometa 3.7 za mchepuo wa barabara ya Kipumbwi kwa kiwango cha lami, mkoani Tanga.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akisisitiza jambo kwa mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation (hayupo pichani), wakati akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange (km 95.2), ikiwemo na kilometa 3.7 za mchepuo wa barabara ya Kipumbwi kwa kiwango cha lami, mkoani Tanga.

Kazi za uchimbaji wa udongo katika barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange (km 95.2), inayojengwa kwa kiwango cha lami zikiendelea, mkoani Tanga.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange (km 95.2), inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Tanga. Barabara hiyo inaunganisha mkoa wa Tanga na Pwani. 

PICHA NA WUU

About the author

mzalendoeditor