Kaimu Meneja Bandari za Ziwa Tanganyika Edward Mabula akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete baadhi ya miundombinu ya bandari iliyokamilika, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Karema Mkoani Katavi.
…………………………………………
Naibu Waziri Uchukuzi, Atupele Mwakibete ametoa wiki mbili kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha bandari mpya ya Karema inaanza kutoa huduma ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria kwa mikoa inayozunguka Ziwa Tanganyika na nchi Jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo mkoani humo ambao umekamilika kwa asilimia 100, Naibu Waziri Mwakibete amesema kukamilika na kutoa huduma kwa bandari hiyo iliyogharimiwa na Serikali kwa fedha za ndani zaidi ya shilingi bilioni 30 kutachochea uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.
“Fedha nyingi zilizowekwa hapa lazima zianze kutumika vitu vilivyobaki ni vichache sana na viko ndani ya uwezo wetu hivyo tuvikamilishe haraka na tuanze kutoa huduma muda hausubiri na mradi umeshakamilika”, amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete amesema pamoja na mradi huo Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 inaendelea na ukarabati wa meli ya MT. Sangara na imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya mbili za abiria na mizigo zitakazotoa huduma katika Bandari za Ziwa Tanganyika na nchi za jirani.
Aidha, Naibu Waziri Mwakibete amewataka TPA kuhakikisha wananchi wa Kata ya Karema wanapewa kipaumbele cha ajira hususani kwa kazi zisizohitaji utaalam sababu ajira hizo zitachochea uchumi wao pia walinzi wa miundombinu hiyo ili iweze kudumu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu .ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuunda vikundi vidogo vidogo ili kutumia fursa ya uwepo wa mradi huo mkubwa kupata ajira za muda mfupi na mrefu wakati itakapoanza kufanya kazi.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula, amesema mradi kwa sasa umeshakamilika na kumuhakikisha Naibu Waziri kuwa kazi zilizobaki ni kufunga umeme kazi itakayofanyika kwa wiki moja pamoja na uletaji wa mitambo ya kuhudumia mizigo.
“Mhe. Naibu Waziri huduma hapa itaanza wakati wowote sababu baada ya kuunganisha umeme, tutafanya majaribio kwa siku chache na baadae tutakamilisha taratibu za uendeshaji na tutaanza kutoa huduma” amesema Kaimu Meneja Edward Mabula.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Mwakibete yuko Mkoani Katavi kwa ziara ya siku mbili ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akitoa maelekezo kwa uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa bandari ya Karema, Mkoani Katavi.
Kaimu Meneja Bandari za Ziwa Tanganyika Edward Mabula akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete baadhi ya miundombinu ya bandari iliyokamilika, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Karema Mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akizungumza na Wananchi wa Kata ya Karema (hawapo pichani) baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa bandari ya Karema, Mkoani Katavi.
Wananchi wa Kata ya Karema wakimsikiliza Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete (hayupo pichani) wakati alipozugumza nao mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa Bandari ya Karema, Mkoani Katavi.
Muonekano Mzani uliopo ndani ya Bandari ya Karema Mkoani Katavi. Mzani huo ni sehemu ya miundombinu iliyojengwa kwenye mradi wa Ujenzi wa Bandari hiyo ambayo kwa sasa umekamilika kwa asilimia mia moja na umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 30.
PICHA NA WUU