Featured

DKT. KOFLER AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA SIKU SABA

Written by mzalendoeditor
Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Bärbel Kofler akisalimiana na Afisa kutoka Ubalozi wa Ujerumani nchini

…………………………….

Na Mwandishi wetu, Dar

Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Shirikisho la Ujerumani, Dkt. Bärbel Kofler amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku saba kuanzia tarehe 13 – 20 August 2022.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Dkt. Kofler amepokelewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga.  

Katika ziara yake nchini, Dkt. Kofler pamoja na mambo mengine, anatarajia kutembelea mradi wa ajira na ujuzi kwa maendeleo ya afrika (E4D) unaofadhiliwa na serikali ya Ujerumani, Kituo cha malezi na mafunzo kwa wasichana wadogo ambao ni wahanga wa biashara haramu ya binadamu kilichopo Kibamba na Hospitali ya CCBRT Jijini Dar es Salaam. 

Maeneo mengine atakayotembelea Naibu Waziri huyo ni pamoja na Kituo cha Afya cha Ngamiani na Hospitali ya Bombo mkoani Tanga, Zahanati ya Mkanyageni Wilayani Muheza, Halmashauri ya Jiji la Tanga, Asasi ya Tree of Hope iliyopo mkoani Tanga pamoja na Hospitali ya KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro.

Katika ziara yake nchini, Waziri Kofler anategemea kukutana na mawaziri wa sekta za afya, sheria, utalii, maendeleo ya jamii, fedha, nishati na maji kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akimueleza jambo Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Shirikisho la Ujerumani, Dkt. Bärbel Kofler walipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Bärbel Kofler akizungumza na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga walipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam

 

About the author

mzalendoeditor