Featured Kitaifa

MAJALIWA: WATUMISHI WA UMMA ZINGATIENI MAADILI

Written by mzalendoeditor

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, katika ukumbi wa Chuo cha Uhasibu (TIA) wakati alipohitimisha ziara ya siku mbili mkoani Singida.

Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

……………………………………………..

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma waondoe urasimu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili wananchi wapate huduma bora.

“Mtu akija mhudumie moja kwa moja, hizi njoo kesho zinakaribisha majadiliano nje ya utaratibu wa Serikali kwa lugha nyepesi rushwa. Tusitengeneze haya mazingira.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Agosti 06, 2022) wakati akizungumza na watumishi wa umma akiwa katika ziara ya kikazi kwenye Manispaa ya Singida.

Amesema watumishi hao wanatakiwa wawatumikie wananchi kwa kuzingatia maadili ya kiutumishi, sheria, taratibu na kanuni wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.

Pia, amewataka watumisho hao watambue makundi mbalimbali katika jamii yakiwemo ya wazee, wanawake na vijana ili wapange namna bora ya kuwahudumia.

“Tuwahudumie bila ubaguzi wa aina yoyote na lazima tuwe na staha kwa kauli tunazozitoa kwao, maelezo yetu yamtie matumaini na kujenga imani kwetu.”

Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza watumishi hao wafanye kazi kwa bidii, uadilifu na maarifa ya hali ya juu. “Tunahitaji kuona ubunifu wenu, maarifa na uadilifu wenu.”

Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa watendaji wa halmashauri wafanye tathmini ya maeneo ya ukusanyaji wa mapato kabla ya kuwakabidhi mawakala kazi ya ukusanyaji.

About the author

mzalendoeditor