Na. WAF- Manyara

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amewatia moyo watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa kuwataka kufanya kazi kwa kutumia kanzi data ili kuleta ufanisi katika ufatiliaji wa mama mjamzito anapofika kituoni kupata huduma mpaka atakapo jifungua.

Dkt. Sichalwe ametoa rai hiyo Mkoani Manyara alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya na kuongea na watumishi ambapo amesema kuwa ujazaji wa taarfa sahihi katika kanzi data utasaidia kufanya tathimini katika kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Katika kupunguza vifo vya mama na mtoto lazima tuwajibike kwa kufanya kazi kwa kufuata miiko ya taaluma na weledi pamoja na kuwa na ushirikiano wa karibu katika kutoa huduma kwa wananchi.

“Hivyo mkidumisha upendo baina yenu watumishi nyote mtaweza kuongea lugha moja na kuleta ufanisi katika kutoa huduma bora kwa wananchi mnao wahudumia na kufanya afya za watanzania kuwa imara”, amesisitiza Dkt. Sichalwe.

Lakini pia amewasihi watumishi wa hospitali hiyo kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na badala yake waimarishe uongozi thabiti wenye mtazamo na fikra chanya zenye kuleta utoaji wa huduma bora.

Dkt. Sichalwe ameitaka bodi ya hospitali kufanya kazi kwa malengo ili kuahakikisha hospitali inapiga hatua kwa kwenda mbele kufuata vipaumbele watakavyo kuwa wamejiwekea ndani ya muda mfupi, kati na mrefu.

Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Serikali, Bi. Ziada Sellah amewasisitiza watumishi hao kutumia fursa iliyotolewa na serikali ya kujiendeleza kimasomo ili kuongeza ujuzi katika taaluma zao.

Pia Bi Ziada amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wagonjwa wanaowahudumia ili kufikia adhima ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ya kutaka upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi na sio bora huduma.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Watoto, Dk.Ahmad Makuwani amewapongeza kwa kuanzisha sehemu maalumu ya kutoa huduma ya wajawazito katika hospitali hiyo.

Previous articleDKT. CHAULA ATAKA UBUNIFU UENDESHAJI MAKAZI YA WAZEE
Next articleWABUNGE NA WATUMISHI WA BUNGE WALIOHITIMU MAFUNZO YA JKT WATAKIWA KUSAIDIA KUPINGA VITENDO VYA UZEMBE KAZINI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here