Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali mara baada ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Tawala kwenye hafla ya Uapisho iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
……………………………………….
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi katika Halmashauri zote kuhakikisha kuwa fedha zinazotolewa na Serikali zinahudumia wananchi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.
Rais Samia amesema hayo katika hafla ya uapisho wa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa iliyofanyika leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rais Samia amesema fedha hizo zitumike katika kusukuma miradi ya maendeleo ya wananchi ikiwemo elimu, maji na afya bila kubadilisha matumizi.
Rais Samia amewataka Madiwani na Makatibu Tawala katika Halmashauri kuacha tabia ya mvutano katika matumizi ya fedha za maendeleo kwa kuwa tabia hiyo inachelewesha ukamilikaji wa miradi.
Vile vile, Rais Samia amezitaka Halmashauri kupitia viwango vya ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ili kuweza kujihudumia na kuweza kujikimu kwa mahitaji ya kiofisi.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ameiagiza Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha kuwa kila ngazi ya Viongozi wanaoteuliwa wanafanyiwa mafunzo ili kukumbushwa kuhusu uwajibikaji kwa wananchi na kulitumikia taifa ipasavyo.