Featured Kitaifa

TAKUKURU DODOMA YAWAFIKISHA MAHAKAMANI WATENDAJI 17 KWA UBADHILIFU WA FEDHA

Written by mzalendoeditor

MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Sosthenes Kibwango,akizungumza na waandishi wa habari  (hawapo pichani) leo Julai 28,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utendaji wa Taasisi hiyo katika robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/22 kati ya Aprili hadi Juni.

MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Sosthenes Kibwango,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari  (hawapo pichani) leo Julai 28,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utendaji wa Taasisi hiyo katika robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/22 kati ya Aprili hadi Juni.

………………………………..

Na Alex Sonna-DODOMA

MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Sosthenes Kibwango,amesema kuwa wamefanikiwa kuwafikisha Mahakamani Watendaji   17 waliofuja fedha za umma kiasi cha sh.milion 179.3.

Hayo ameyasema leo Julai 28,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, Kibwengo amesema kuwa watendaji hao walichunguzwa na tayari mashauri 15 kuhusiana na ubadhilifu huo yamefikishwa mahakamani.

Kibwengo amesema kuwa TAKUKURU  imefanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi 77 ya maendeleo ya sh.bilion 19.6  katika sekta ya maji,afya,elimu na ujenzi.
Aidha amesema kuwa  kati ya miradi hiyo 58 yenye thamani ya sh. billion 10 ilitekelezwa kwa fedha za UVIKO 19.
“Ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ni endelevu ambapo elimu namna ya kuondokana na mianya ya rushwa hutolewa na ushauru wa kuboresha maeneo yenye mapungufu umetolewa,ufuatiliaji hujumuisha wataalamu kutoka idara nyingine za serikali,
”Kuna suala la kucheleweshwa kukamilika kwa baadhi ya miradi kinyume na mikataba jambo ambalo linapunguza  ufanisi na kuongeza gharama.
Hata hivyo Kibwengo amesema kuwa TAKUKURU Dodoma imefanikiwa kufanya mikutano ya hadhara 42 ambapo elimu ilitolewa na kero za rushwa zilisikilizwa na kutatuliwa na kufanya maonesho mawili,vipindi vya redio 15  na kuandaa makala maalumu kuhusu rushwa .
Pia amesema kuwa TAKUKURU kwa ilishirikiana na Tume ya Haki za Binadamu  na Utawala Bora katika siku 10 kuelekea siku ya mtoto wa Afrika kutoa elimu ya rushwa ya ngono mashuleni na kupitia vipindi vya redio.
“Kupitia ufuatiliaji wetu wa fedha za serikali tumefanikiwa kuokoa fedha sh.milion 10.9zilizokusanywa kupitia mashine za POS ambazo zilikuwa mikononi mwa watu,”amesema
Kibwengo amesema kuwa ni wajibu wa wananchi wote kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na wanapoona inacheleweshwa makusudi ili kuongeza gharama watoe taarifa.
Aidha amewataka wananchi kushiriki katika vita hivyo vya rushwa kwa kuhimiza viongozi wa vijiji na mitaa kuitisha mikutano ili wahoji na wadadisi mapato na matumizi ya miradi mbalimbali katika maeneo yao.
”Vita ya rushwa itafanikiwa kama wananchi watabadili mtazamo na kuona ni wajibu wao kutoa taarifa za viashiria vya rushwa vinapojitokeza katika mitaa na vijiji vyao.”amesisitiza

About the author

mzalendoeditor