Featured Kitaifa

WAZIRI MKENDA ASHUHUDIA UWEKAJI SAINI RASIMU YA MPANGO KAZI WA UTEKELEZAJI WA MAKUBALIANO KWENYE ELIMU KATI YA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI

Written by mzalendoeditor

Utekelezaji wa Hati ya Makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini kwenye maeneo mbalimbali ya elimumsingi umeanza kwa kasi ambapo leo Julai 28, 2022 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameshuhudia uwekaji saini wa rasimu ya Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Makubaliano hayo.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam mara baada ya kushuhudia tukio hilo Waziri Mkenda amesema hatua hiyo inatoa mwelekeo wa jinsi ya kushirikiana baina ya nchi hizo mbili kwenye elimu hususan ufundishaji wa lugha ya Kiswahili pamoja na mitaala.

Amesema lengo la uwekaji saini huo ni kila upande kati ya Tanzania na Afrika Kusini ujifunze kwa mwenzake kusaidia kuendeleza Kiswahili.

“Baada ya kusaini Hati ya Makubaliano Julai 7, 2022 tulikubaliana na Waziri mwenzangu anayeshughulika na Elimu nchini Afrika Kusini kwamba tusiwe na hati ya makubaliano tu halafu tukaiweka kabatini, bali timu zikutane kuweka mpango kazi wa utekelezaji,” amesema Prof. Mkenda

Alisema kikubwa kwenye makubaliano hayo sio kufundisha Kiswahili tu lakini kuweka msukumo katika kuendeleza Kiswahili katika Bara la Afrika.

Aliongeza kuwa Tanzania ina wajibu mkubwa wa kukuza Kiswahili na kuhakikisha kinasambaa katika nchi zote Afrika.

About the author

mzalendoeditor