Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI SAGINI ATEMBELEA KITUO CHA POLISI KEGONGA, AKUTA ASKARI WAPO KITUONI.

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ametembelea na kukagua Kituo cha Polisi Kegonga kilicholalamikiwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya ubora wa kituo hicho pamoja na lalamiko la kuhamishwa askari wa Polisi wa kituo hicho.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akizungumza na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waiatara baada ya ukaguzi wa Kituo cha Polisi Kegonga na kuridhishwa na uwepo wa askari wa Jeshi la Polisi kituoni.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kegonga wanaoishi baada ya ukaguzi wa Kituo cha Polisi cha Kegonga

……………………………………
 
Na Mwandishi wetu,
 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini ametembelea na kukagua Kituo cha Polisi Kegonga kilichopo, Kijiji cha Kegonga, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara ili kuangalia kituo hicho kilicholalamikiwa kwenye Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania juu ya ubora wa kituo hicho pamoja na lalamiko la kuhamishwa kwa askari wa kituo hicho.

Katika ziara hiyo aliambatana na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kegonga baada ya kukagua kituo hicho, Naibu Waziri Sagini amewataka wananchi wa Kijiji cha Kegonga kushirikiana na Serikali ya Wilaya katika ujenzi wa kituo hicho aidha Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi huo.

Hata hivyo Mbunge wa Tarime Vijijini, Mh. Mwita Waitara ameahidi kutoa kiasi cha shillingi milioni kumi kwenye mfuko wa jimbo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
 
“Ni jukumu la kila mwananchi kushiriki katika ulinzi shirikishi. Niwaombe mshirikiane na Serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime muanze ujezi alafu Wizara kupitia Jeshi la Polisi itajumuika nanyi katika ujenzi wa kituo hicho”
 
Naibu Waziri Sagini aliyasema hayo tarehe 20/07/2022 alipotembelea kituo cha Kegonga ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Mara.
 
Aidha Naibu Waziri Sagini amefurahi kukuta askari wa Jeshi la Polisi katika Kituo hicho na kuwahakikishia wananchi wa Kijiji cha Kegonga kuwa askari wa kituo hicho hawakuhamishwa bali walikuwa kwenye jukumu la kusimamia mitihani.

“Nimefurahi kukuta Askari polisi wapo kituoni,OCS yupo pamoja na wasaidizi wake.Na wamesema walikuwa wanasimamia mitihani ndio maana baadhi ya askari hawakuwepo kituoni” alisema

Akitoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Sagini amewakumbusha wananchi wa Kijiji cha Kegonga kushiriki kwenye Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022 itakayosaidia katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya nchi.
 
“Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu sana katika kupanga mipango ya maendeleo nchini. Naomba niwakumbushe kushiriki katika sensa ifikapo Agosti 23 mwaka huu”
 
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Sagini pia alitembela na kukagua Kikosi cha Polisi Wanamaji Shirati, iliyopo wilayani Rorya ili kufahamu utendaji kazi wao pamoja na changamoto zinazowakabili na kuahidi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itashughulikia changamoto yao ya vifaa zitakazowasaidi kulinda wavuvi wa Tanzania.
 

About the author

mzalendoeditor