Featured Kitaifa

KIJIJI CHA IKINA GEITA KUONDOKANA NA ADHA YA UKOSEFU WA MAJI SAFI NA SALAMA

Written by mzalendoeditor

NA. Costantine James, Geita.

WANANCHI wa kijiji cha Ikina kata ya Bukoli mkoani Geita wameipongeza serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Geita kwa kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji safi na salama katika kijiji cha ikina.

Wamesema hayo leo 21.7.2022 katika kijiji cha Ikina baada ya mradi wa maji safi na salama katika kijiji hicho kuwekewa jiwe la msingi na Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa ndugu Sahili Nyanzabara wamesema Kabla ya mradi huo walikuwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama.

Wamesema changamoto kubwa iliyokuwa inawakabili nikufata maji umbali mrefu hali iliyokuwa inasababisha kutumia mda mrefu kufata maji huku wakibeba ndoo za maji kichwani kwa umbali mrefu na hilo limekuwa ni chanzo cha mifarakano katika ndoa ndoa zao.

Wameshukuru kukamilika kwa mradi huo kwani sasa wanapata huduma ya maji safi na salama kalibu na kwa urahisi zaidi na wameipongeza serikali kwa kuwatua mama ndoo kichwani.

Meneja wa RUWASA wilaya ya Geita Mhandisi Sande Batakanwa amesema mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi julai 2021 na kukamilika mwezi juni 2022 na utahudumia wakazi wapatao 2,400 kupitia vituo vya kuchotea maji na wateja wa majumbani.

Mhandisi Sande amesema gharama za mradi huo mpaka kukamilika kwake ni milioni 129.2 na mradi huo utasaidia kupunguza magojwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama kama vile kuhara, Homa ya matumbo na Kipindupindu.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa ndugu Sahili Nyanzabara ameipongeza RUWASA kwa kutekeleza vyema mradi huo kwani wametimiza vyema adhima ya serikali ya kumtuma mama ndoo kichwani.

Amesema kwa asilimia zaidi ya 95% RUWASA nchini inatekeleza vyema miradi ya wananchi kwa kukamilika na kuanza kutoa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi.

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA mkoa wa Geita Mhandisi Jabiri Kayila amewataka wananchi wa kijiji hicho kuutunza mradi huo kama mali yao ili uweze kutumika kwa mda mrefu.

Amesema wao kama RUWASA mkoa wa Geita jukumu lao nikutekeleza miradi kwa ufanisi zaidi ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao hivyo wananchi wanapaswa kuwa walinzi katika miradi ya maji inayotumia pesa nyingi kwa ajiri yao.

About the author

mzalendoeditor