Featured Kitaifa

‘WADAU MSIBAKI NYUMA SAFARI YA MAHAKAMA MTANDAO’-JAJI MKUU

Written by mzalendoeditor

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi alipokuwa katika ziara ya kikazi jana alipotembelea Divisheni hiyo iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi pamoja na Majaji wa Divisheni ya Kazi (katika picha) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake katika Divisheni hiyo jana tarehe 18 Julai, 2022. Katikati ni Mhe. Katarina Revocati Mteule, kushoto ni Mhe. Biswalo Mganga na kulia ni Mhe. Augustine Rwizile.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza jambo katika Mkutano kati ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi akitoa hotuba ya utendaji wa Divisheni hiyo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) wakati Jaji Mkuu alipotembelea Mahakama hiyo kwa ziara ya kikazi.

Baadhi ya Viongozi kutoka makao makuu pamoja na sehemu ya Watumishi wa Divisheni ya Kazi wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania (hayupo katika picha) wakati alipotembelea Divisheni hiyo jana tarehe 18 Julai, 2022.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akizungumza na Watumishi wa Divisheni ya Kazi. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi na kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani (T), Bw. Solanus Nyimbi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akisisitiza jambo. Katikati ni Jaji Kiongozi wa Mahakaama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani na kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Kevin Mhina.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Bw. Samson Mashalla akizungumza jambo katika Mkutano kati ya Jaji Mkuu pamoja Watumishi wa Divisheni hiyo.

Jaji  Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Elinaza Luvanda akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Divisheni hiyo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipofanya ziara ya kikazi katika Mahakama hiyo jana tarehe 18 Julai, 2022.

Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi wakiwa katika Mkutano na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipofanya ziara katika Divisheni hiyo.

Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Immaculata Banzi akimkabidhi zawadi maalum Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 18 Julai, 2022 alipotembelea Divisheni hiyo kwa ziara ya kikazi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akifurahia zawadi aliyopewa na Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (waliosimama).

……………………………………….

 Na Magreth Kinabo na Mary Gwera- Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kwamba wadau wa Mahakama ya Tanzania wasibaki nyuma katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wakati huu Mahakama inapoelekea kwenye Mahakama mtandao ‘e-Judiciary’.

Akizungumza na Watumishi wa  Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Jijini Dar es Salaam jana tarehe 18 Julai, 2022 akiwa katika ziara ya kikazi, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa, Mahakama imewekeza katika  matumizi ya TEHAMA, hivyo, Wadau pia wanatakiwa kuondoka kwenye matumizi ya karatasi kwenda na kidijitali.

“Katika utoaji huu wa haki kidijitali ni muhimu kuwavuta wadau wetu ili wote tuwe na safari moja ya kwenda kwenye Mahakama Mtandao, hakuna ambaye atakuwa na nafasi ya kubaki nyuma, wadau wote wanatakiwa kuingia katika mfumo huu,” amesema Jaji Mkuu huku akiwataja baadhi ya wadau hao kuwa ni Jeshi la Polisi, Magereza Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) na wengine.

Amesema matumizi ya TEHAMA ni nyenzo muhimu kwa kuwa yanapunguza changamoto ya ukosefu wa watumishi na rasilimali fedha. Amebainisha kuwa lengo la ziara yake katika Divisheni hizo ni kukagua matumizi ya TEHAMA hivyo zinapaswa kuwa za mfano wa kuigwa katika matumizi hayo na kuwa walimu kwa wengine katika kanda zingine.

“Unapoanzisha shauri kidijitali ni vizuri kuendelea nalo kidijitali hadi linapofikia kwenye hatua ya uamuzi, hili ni eneo ambalo linahitaji mafunzo ili tuweze kufika huko,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu aliongeza kwamba,  ni vema mafunzo kuhusu Mahakama Mtandao kila mtumishi  akapatiwa na wadau wakahusishwa kwa kuwa ni suala ambalo halikwepeki ili kuweza kuwa na uelewa wa pamoja wa kuondoka kwenye matumizi ya karatasi. Pia alisema faida ya matumizi ya teknolojia hiyo inapunguza mlundikano wa mashauri, kuongeza ufanisi wa kazi, uwazi na utoaji wa haki iliyo bora na yenye tija.

Amefafanua kuwa hivi sasa Mahakama iko katika hatua nzuri ya kuandaa programu ya kuweza kutafsiri lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili cha kisheria na kutumia teknolojia/akili bandia, hivyo programu hiyo itakuwa inafanya kazi yenyewe na hakuna haja ya kutafuta kamusi na kumpunguzia Jaji au Hakimu kazi ya kuandika.

Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi  amesema kuanzia Desemba, 2020 hadi kufikia Desemba 2021 mashauri yaliyobakia kufikia Desemba 2020 yalikuwa ni 2,124, yaliyosajiliwa  2021 ni 1,537. Mashauri yaliyoamuliwa 2021 ni 2,135 na mashauri yaliyobakia Desemba 2021 ni 1,526.

Ameongeza kuwa mashauri yaliyobakia kufikia tarehe 30, 2021 ni 2,071, mashauri yaliyosajiliwa kuanzia tarehe 01 Julai, 2021 mpaka tarehe 15 Julai, 2022 ni 1,736 na mashauri yaliyoamuliwa kuanzia tarehe 01 Julai, 2021 mpaka tarehe 15 Julai, 2022 ni 3,014 sawa na asilimia 174 ya mashauri yaliyofunguliwa.  Mashauri yaliyobaki hadi kufikia Julai 15, 2022 ni 793. Mashauri mlundikano ni 42 sawa na asilimia 5.3 ya mashauri yaliyopo.

Jaji Maghimbi amesema kuwa  ili kuondokana na mlundikano wa mashauri, kuanzia Julai 2021 hadi Juni 30, 2022, Divisheni hiyo imefanya vikao maalum 21, ambapo  mashauri 643 yalisikilizwa na kumalizika.

Akizungumzia kuhusu mifumo ya kielektroniki, amesema Mahakama hiyo inatumia mifumo yote ya kielektroniki iliyowekwa na Taasisi katika kuboresha na kurahisisha utendaji kazi wa shughuli za kimahakama.  

“Matumizi ya TEHAMA yamesaidia katika upatikanaji wa haki kwa wakati , kupatikana kwa taarifa za mashauri ikiwa ni pamoja na ujumbe wa taarifa za mashauri kutumwa kwa wadaawa mara baada ya kesi kutoka mahakamani,” amesema huku akiongeza kuwa, katika kipindi cha Julai 2021 hadi kufikia Juni, 2022 jumla ya hukumu 705 zimepandishwa kwenye mfumo wa TanzLII kati ya uamuzi na hukumu 737 ambayo yametolewa katika kipindi hicho sawa na asilimia 95.6.

Naye; Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Elinaza Luvanda akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo, amesema mashauri yote yanasajiliwa kwa njia ya kielektroniki bila kujali ukubwa wake mfano shauri Na. 6/2022 lenye makosa 752, maelezo ya mashahidi 80 na vielelezo vya nyaraka 1, 055.

Jaji Luvanda amesema kuwa, wakati Divisheni hiyo ilipoanza kutekeleza majukumu yake, ilianza kwa kusikiliza mashauri ya maombi ya dhamana pamoja na mashauri ya msingi ya uhujumu uchumi. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016 hadi 2018 Mahakama hiyo katika masjala zake zote ilisajili jumla ya mashauri 501, kati ya hayo mashauri 383 ni ya maombi ya dhamana sawa na 76.44% na mashauri ya msingi ya uhujumu uchumi yalikuwa 118 sawa na 23.55%.

Hivyo ameongeza kuwa, kuanzia mwaka 2019 Mahakama hiyo imeendelea kusajili mashauri ya msingi tu yaani mashauri ya uhujumu uchumi pamoja na yale ya maombi mbalimbali ya uhujumu uchumi. Kwa kipindi cha kuanzia 2019 hadi tarehe 15 Julai, 2022 yamesajiliwa jumla ya mashauri 266 katika masjala zote. Mashauri 223 yakiwa ya uhujumu uchumi sawa na asilimia 83.83 na mashauri 43 ya maombi mbalimbali ya uhujumu uchumi sawa na asilimia 16.16.

“Idadi ya usajili wa mashauri ya uhujumu uchumi imeongezeka kutoka 118 kwa kipindi cha kati ya mwaka 2016 na 2018 hadi kufikia mashauri 266 kwa kipindi cha kuanzia 2019 hadi tarehe 15 Julai, 2022 sawa na ongezeko la asilimi 44, hivyo makosa yanayosajiliwa kwa wingi ni makosa ya usafirishaji wa madawa ya kulevya, utakatishaji fedha, ugaidi, upatikanaji wa nyara za serikali, na kusababisha hasara. Kwa mwaka 2019 na 2020 mengi yalikuwa mashauri ya uhujumu uchumi na wizi wa fedha za umma,” ameeleza Jaji Luvanda.

Akizungumzia kuhusu hali ya mashauri ya sasa amesema hadi kufikia Desemba, 2021, mashauri yaliyobaki mahakamani yalikuwa 70 pekee, mashauri ya uhujumu uchumi yalikuwa 63 na mashauri ya maombi yalikuwa sab ana kuanzia Januari 2022 hadi tarehe 15 Julai, 2022 yamesajiliwa jumla ya mashauri 43 katika masjala zote, ambapo kati ya hayo, mashauri 34 ni ya uhujumu uchumi na tisa ni maombi.

Aidha, amesema  kuanzia Januari 2022 hadi tarehe 15 Julai, 2022 yamesikilizwa mashauri 48 katika masjala zote, ambapo kati ya hayo, mashauri 35 ni ya uhujumu uchumi na mashauri 13 ni maombi. Hivyo hadi kufikia tarehe 15 Julai, 2022 mashauri yaliyobaki mahakamani ni 65. Kati ya hayo mashauri 62 ni ya uhujumu uchumi na matatu ni maombi mbalimbali.

Katika ziara yake ya kikazi Jaji Mkuu ametembelea Mahakama Kuu-Kituo cha Usuluhishi, Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Mahakama Kuu-Divisheni ya Biashara, Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi na anatarajia kuhitimisha ziara yake tarehe 20 Julai kwa kutembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Temeke.

About the author

mzalendoeditor