Featured Kitaifa

BALOZI ZA TANZANIA ZATAKIWA KUONGEZA KASI YA KUTANGAZA FURSA ZA KIUCHUMI ZILIZOPO NCHINI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ametoa wito kwa
Mabalozi wa Tanzania nje kuongeza kasi katika utekelezaji wa Diplomasia ya
Uchumi hususan katika kutangaza utalii, kuvutia wawekezaji na kuhamasisha
biashara baina ya Tanzania na nchi mbalimbali duniani.

 

Balozi Mulamula ametoa wito
huo alipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika
Kusini hivi karibuni na kuzungumza na Watumishi katika Ubalozi huo.


Mhe. Balozi Mulamula ambaye
alipokelewa ubalozini hapo na Balozi wa Tanzania nchini humo, Meja Jenerali Mstaafu, Mhe.
Gaudence Milanzi amesema kuwa, tangu Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania aingie madarakani, ameonesha kwa vitendo na kasi ya
hali ya juu katika kutangaza fursa mbalimbali zinazopatikana nchini ikiwemo
utalii, uwekezaji, biashara na utamaduni na kuwataka Mabalozi kwenda sambamba
na kasi hiyo ya Mhe. Rais Samia ili kupata matokeo tarajiwa katika kukuza
uchumi wa nchi.

 

“Nazipongeza Balozi zote kwa
jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanyika katika kutangaza fursa mbalimbali
zilizopo nchini. Kasi nyumbani ni kubwa, hivyo nawasisitiza na ninyi Mabalozi
wetu kuongeza kasi ili kwenda pamoja na kasi ya Mhe. Rais wetu ambaye amekuwa
mstari wa mbele katika kuitangaza nchi,” alisema Balozi Mulamula.

 

Kadhalika amesema kuwa
Wizara inaendelea kuimarisha mifumo mbalimbali ikiwemo Diplomasia ya Umma na
Diplomasia ya Kidijitali ili kuwezesha nchi kujitangaza zaidi na kurahisisha
mawasiliano na kwamba ataendelea kufanya vikao kazi na Mabalozi kila baada ya
miezi mitatu ili kukumbushana masuala mbalimbali katika kuboresha utendaji kazi.

 

Akizungumzia utendaji katika
Ubalozi wa Afrika Kusini, Waziri Mulamula alimpongeza Balozi Milanzi kwa
kujenga umoja miongoni mwa Watumishi wa Ubalozi huo na kusisitiza kuendelea
kutekeleza majukumu yao kwa weledi, nidhamu, ushirikiano, uadilif na ubunifu.

 

“Namshukuru Balozi kwa
kujenga umoja miongoni mwenu. Nasisitiza ushirikiano, nidhamu, uadilifu, muwe
wabunifu na  mfanye kazi zenu kwa weledi.
Naomba mzingatie kuiwakilisha nchi vizuri kwani mmebeba taswira ya nchi”
alisisitiza Balozi Mulamula.

 

Pia, Waziri Mulamula
aliupongeza ubalozi huo kwa kulipa kipaumbele suala la Diaspora ambao idadi yao
ni kubwa nchini humo na kuwasisitiza kuendelea kuwashirikisha Diaspora katika
kuchangia maendeleo ya nchi. 

 

Vilevile, Mhe. Waziri
Mulamula alitumia fursa ya kuwa nchini humo kutembelea nyumba mbili
zinazomilikiwa na Serikali ili kuona hali ya nyumba hizo kwa ajili ya kutoa
mapendekezo ya jinsi ya kuziboresha ili kuiwezesha Serikali kunufaika nazo kama
vitega uchumi. Nyumba moja kati ya hizo inamilikiwa na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar na nyingine inamilikiwa na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

 

Kwa upande wake Balozi
Milanzi, alimshukuru Mhe. Balozi Mulamula kwa kutenga muda na kutembelea
Ubalozi huo na kuahidi kutekeleza maelekezo yote aliyotoa kwao. 

 

Mhe. Balozi Mulamula yupo
nchini Afrika Kusini akiongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 24 wa
Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa,
Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) utakaofanyika
jijini Pretoria, Afrika Kusini tarehe 19 Julai, 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi. Mhe. Waziri Mulamula yupo nchini humo akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kawaida wa 24 wa Kamati ya Mawaziri wa SADC wa Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama utakaofanyika Pretoria tarehe 19 Julai 2022. Wanaoshuhudia ni Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi na Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga
 

 
 

 

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi akimkaribisha Mhe. Balozi Liberata Ubalozini kwa ajili ya kuzungumza na Watumishi wa Ubalozi huo  
Mhe. Waziri Mulamula akizungumza na Watumishi wa Ubalozi (hawapo pichani) wa Tanzania nchini Afrika Kusini

 

 Mhe. Balozi Mulamula akiendelea na mazungumzo na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini alipotembelea ubalozi huo hivi karibuni
                     

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma M. Rajab ambaye aliambata na Waziri Mulamula Ubalozini hapo naye akichangia jambo wakati wa mazungumzo hayo
Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma (kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Balozi Agnes Kayola wakifuatilia mazungumzo kai ya Mhe. Balozi Mulamula na Watumishi wa Ubalozi (hawapo pichani)
Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akiwa na Afisa wa Ubalozi Mwandamizi, Bw. Peter Shija wakifuatilia kikao kati ya Mhe. Waziri na Watumishi wa Ubalozi huo

 

Sehemu ya Watumishi wa Ubalozi wakiwa kwenye kikao na Mhe. Balozi Mulamula. Kulia ni Mkuu wa Utawala Ubalozini, Bw. Deogratius Dotto akiwa na Bi. Happiness Godfrey, Afisa katika Ubalozi huo
 Sehemu nyingine ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini. Kushoto ni Bibi Faith Masaka na Bw. Rweyemamu

 Kikao kikiendelea

                         

 

Afisa katika Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Bi. Happiness Godfery akimkabidhi zawadi ya ua Mhe. Balozi Mulamula mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo jijini Johannesburg. Mhe. Balozi Mulamula yupo nchini humo kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 24 wa Kamati ya Mawaziri wa SADC

 

Mhe. Balozi Mulamula akisalimiana na Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Bw. Deogratius Dotto wakati wa mapokezi yake mara baada ya kuwasili nchini humo. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Mawasiliano, Balozi Kasiga na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Bw. Peter Shija

Mhe. Balozi Mulamula akipata maelezo kuhusu moja ya nyumba zinazomilikiwa na Serikali zilizopo nchini Afrika Kusini alipozitembelea kwa ajili ya kufanya tathmini ya nyumba hizo.  Kati ya nyumba hizo mbili,  moja inamilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inamilikiwa na ATCL

 

Mhe. Waziri Mulamula  kwa pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Fatma wakiangalia nyumba hiyo (haipo pichani)

 

Mhe. Balozi Mulamula akipata maelezo kuhusu nyumba inayomilikiwa na ATCL alipotembelea eneo hilo jijini Johannesburg

About the author

mzalendoeditor