Featured Kitaifa

TANZANIA KUTUMIA FURSA ZA UWEKEZAJI KUTOKA BENKI YA AFREXIM

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiagana na Rais wa Benki ya Afrexim, Prof. Benedict Oramah, baada ya kukamilika kwa mkutano kati yao, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiahidi kutumia fursa zilizopo katika Benki ya Afrexim alipokutana na  Rais wa Benki hiyo, Prof. Benedict Oramah, jijini Dodoma.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza jambo wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia) na Rais wa Benki ya Afrexim, Prof. Benedict Oramah (hayupo pichani), jijini Dodoma.

Rais wa Benki ya Afrexim, Prof. Benedict Oramah, akieleza fursa za kiuchumi zilizopo katika Benki yake wakati wa Mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba

Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Rais wa Benki ya Afrexim, Prof. Benedict Oramah, uikiendelea jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa sita kushoto) na Rais wa Benki ya Afrexim, Prof. Benedict Oramah (wa tano kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Tanzania na Benki ya Afrexim, jijini Dodoma

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)

……………………………..

Na. Peter Haule, WFM, Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba amemuahidi Rais wa Benki ya Afrexim kuongeza mtaji wa ziada katika Benki hiyo ambayo Tanzania inamiliki hisa ili iwe na wigo mpana wa kuendelea kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Dkt. Nchemba ametoa ahadi hiyo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Afrexim, Prof. Benedict Oramah, ambapo walijadili masuala kadhaa likiwemo  fursa zinazotolewa na Benki hiyo.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali itashirikiana na Benki hiyo ambayo kuanzishwa kwake kulikuwa na lengo la kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika nchi za Afrika.

“Tunatekeleza dira ya Mhe. Rais ya kuweza kuvutia uwekezaji, kuendeleza maeneo mahususi ya uwekezaji (EPZ) pamoja na upande wa Zanzibar ambayo inakusudiwa kutengeneza ajira nyingi kwa vijana ili pato la mtanzania mmojammoja liongezeke na kuweza kupunguza umasikini”, alieleza Dkt. Nchemba.

Aidha Dkt. Nchemba amesema kuwa Tanzania inaahidi kuendelea kufanyakazi pamoja na ofisi ya Rais huyo kwa kuzishirikisha Wizara zake, ikiwemo ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo na Afya ili kuweza kutumia fursa zilizobainishwa na Benki hiyo.

Kwa upande wake Rais wa Benki ya Afrexim, Prof. Benedict Oramah, alisema kuwa Benki yake inafursa nyingi zikiwemo za mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya na viwanda.

Alizitaja fursa nyingine ambazo Tanzania inaweza kuzipata kuwa ni pamoja na  kuwezesha Kanda maalum za kiuchumi, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo pamoja na uwekezaji katika hisa kupitia taasisi za fedha.

About the author

mzalendoeditor