Featured Kitaifa

MAJALIWA: TCU ONGEZENI UDHIBITI WA UBORA WA VYUO VIKUU

Written by mzalendoeditor

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia mfano wa jengo, kwenye banda la Chuo Kikuu cha Ardhi, wakati alipofungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam .

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza Watendaji wa Wizara ya Elimu na Tume ya Elimu ya Juu Tanzania (TCU), baada ya kufungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam . Julai 19, 2022. Kutoka kulia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Profesa Charles Kihampa, Mwenyekiti wa Bodi Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Profesa Penina Muhando na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Profesa James Mdoe. 

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia ndege isiyokua na rubani inayotumika kupiga picha za anga kwa ajili ya kuandaa ramani za msingi zinazowezesha kupanga miji, wakati alipofungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam .

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia kompyuta mpakato inayotumia mwanafunzi ya Chuo Kikuu Huria, mwenye uono hafifu Bernadeta Msigwa kwa kuandikia vitabu, wakati alipofungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam . 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea ngao ya shukrani kwa kufungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam . Julai 19, 2022. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Profesa Charles Kihampa. 

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi waliohudhuria katika ufunguzi wa Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia, yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam . Julai 19, 2022.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…………………………

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) iongeze jitihada katika udhibiti wa ubora wa vyuo vikuu nchini ili kuhakikisha kuwa azma ya kuwa na mitaala inayojibu mahitaji ya soko la ajira inatimia. “Pamoja na kusimamia taaluma, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, pia iongeze jitihada katika kusimamia masuala ya utafiti na ushauri katika vyuo vikuu ili kuvifanya viwe chachu ya maendeleo na suluhisho la changamoto mbalimbali za maendeleo ya jamii yetu na Taifa kwa ujumla.”

Ametoa wito huo leo (Jumanne, Julai 19, 2022), wakati akifungua Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia kwenye viwanja vya Manazi Mmoja jijini Dar Es Salaam.

Ametoa wito kwa taasisi zote za elimu ya juu kuendelea kufanya mapitio ya mitaala iliyopo kwa kuzingatia miongozo iliyopo ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.  Waziri Mkuu amesema taasisi za elimu ya juu ambazo ni wazalishaji wa maarifa na ujuzi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa, hazinabudi kuwa mbele ya wakati siku zote ili kuhakikisha kuwa zinabuni na kuanzisha programu mpya zinazokwenda na wakati.

“Taasisi za Elimu ya Juu na zile za Utafiti na Maendeleo zishirikiane kwa karibu na sekta binafsi, hususan viwanda, na kuweka utaratibu wa kuendeleza teknolojia zinazozalishwa nchini na kuhamasisha matumizi yake ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa sekta ya elimu ya juu imeendelea kukua kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pamoja na kushirikiana na sekta binafsi.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika utoaji wa elimu kwa ngazi zote nchini, kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya Juu huku akibainisha kuwa kati ya vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 47 vilivyopo hivi sasa, 28 vinamilikiwa na Sekta binafsi.

“Serikali inatambua na kuthamini sana mchango wenu katika kuwahudumia Watanzania wote kwa kutoa elimu bora bila ubaguzi wa aina yoyote. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza Serikali ishirikiane kwa karibu na sekta binafsi na kuendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuharakisha azma yake ya kuleta maendeleo kwa wananchi wote.”

Aidha, ameagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuendelea kusimamia na kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhusu mwenendo wa baadhi ya asasi zilizosajiliwa kuratibu wanafunzi wanaokwenda kusoma vyuo vikuu nje ya nchi.

“Ninatoa wito kwa wananchi wote wanaokwenda kusoma katika vyuo vikuu nje ya nchi kutumia Asasi hizo zilizosajiliwa ili kuepuka hasara ya kutapeliwa fedha zao, na hata kupelekwa katika programu na vyuo visivyotambulika na nchi na hata mamlaka za nchi husika.”

Waziri Mkuu ametoa wito kwa Taasisi za Elimu ya Juu na zile za Utafiti na Maendeleo zishirikiane kwa karibu na sekta binafsi, hususan viwanda, na kuweka utaratibu wa kuendeleza teknolojia zinazozalishwa nchini na kuhamasisha matumizi yake ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amempongeza Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria, Bernadeta Msigwa, kwa kuandika kitabu ambaye ameweza kujifunza kutumia teknolojia zinazotumiwa na watu wenye ulemavu wa uono hafifu na kumuahidi kumuwezesha kupata ajira katika shule ya watu wenye mahitaji maalum ili aweze kutumia ujuzi alioupata kwa wanafunzi wengine wa Kitanzania.

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Profesa Penina Muhando, amesema maonesho hayo yana lengo la kukuza ushirikiano baina ya Wao kama wasimamizi wa Elimu ya Juu na Taasisi zinazotoa huduma pamoja na kutoa fursa kwa wananchi kujifunza kwa pamoja huduma zinazotolewa na Taasisi hizo.

About the author

mzalendoeditor