Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Mashindano ya riadha yajulikanayo kama NBC Dodoma marathoni yanatarajiwa kufanyika Julai 31, 2022 Jijini Dodoma huku yakishirikisha wanariadha zaidi ya 5000 na zaidi ya shilingi milioni 65 zitatolewa kwa washindi wa mbio hizo na fedha zitakazokusanywa zitakwenda kusaidia kutibu wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi katika taasisi ya saratani ya Ocean Road Jijini Dar es saalam.
Akizungumza leo Julai 18,2022 na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuelekea maandalizi ya mbio za marathoni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema maandalizi kwa kiasi kikubwa yamekamilika na kuwataka wanariadha kuendelea kujiandikisha ili kushiriki mbio hizo.
“Mashindano haya kwa sasa yameboreshwa kwa kiasi kikubwa tofauti na miaka mingine na sisi kama mkoa tumejiandaa kupokea wageni mbalimbali watakaokuja kushiriki mashindano hayo” amesema Mtaka.
Amesema mshindi katika mashindano hayo kwa kilomita 42 mshindi atapokea kiasi cha shilingi milioni 8 lakini endapo mshindi atakuwa ni mtanzania atapokea kiasi cha shilingi milioni 10 ikiwa ni kuamsha ali kwa wazawa kushiriki katika mashindano ya riadha.
“kama mshindi wa kilomita 42 atakuwa ni mzawa basi atapokea kiasi cha milioni 10 kama zawadi vivyo hivyo kwenye kilomita 21 mshindi wa jumla atapata milioni 4 lakini kama atapata mzawa atazawadiwa milioni 5 watanzania wachangamkie fulsa hii nzuri sana kwa watanzania” amesema.
Pia amewataka waandaaji wa mashindano kutowazuia wakimbiaji wanaotoka katika mataifa mengine kwani hao watasisimua ali na kuwapa changamoto wazawa nao kushiriki kikamilifu katika mbio hizo na kuwapa uzoefu wazawa kuweza kushindana kimataifa.
“Tumeona jana kwenye mashindano ya dunia kuna mtanzania alishika nafasi ya 7 kwahiyo asingekuwa anapata changamoto kwa wakimbiaji wa nje asingeweza kupata hiyo nafasi na sisi tunataka kwenda kimataifa wengi zaidi na mbio hizi za NBC Dodoma marathon tunataka ziwe za kimataifa” amesema.
Mtaka amewataka wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuzipokea mbio hizo kam a dirisha la kiuchumi na kujiandaa na kuendana na ongezeko la mahitaji ya kijamii kwa kuwa washiriki zaidi ya 7000 watahitaji huduma mbalimbali ambazo itakuwa fulsa kwa wakazi wa mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Theobald Sabi amesema Benki hiyo inafuraha kuandaa tena mbio hizo ikiwa ni mwaka wa tatu kuandaa mbio hizo na kwa mwaka huu kuna mabadiliko makubwa sana na zawadi nono.
“dhamira yetu ni kukusanya zaidi ya shilingi milioni 200 na kuzipeleka katika taasisi ya saratani ya Oceon Raod katka kusaidia mapambano dhidi ya salatani ya shingo ya kizazi kwa wanawake hapa nchini” amesema Sabi.
Amesema jambo la kutia moyo ni kwamba saratani hii inazuilika na kutibiwa iwapo itagundulika mapema na hili ni jukumu letu kwa pamoja kuiunga mkono serikali katika mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi.
Sabi pia amebainisha kuwa kwa miaka miwili iliyopita mbio za NBC Dodoma Marathoni zimekuwa na mafanikio makubwa na kufanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 300 ambazo zilisaidia wanawake zaidi ya 9000 kupima ambao kati yao wanawake 550 waligundulika kuwa na saratani na mpaka sasa wanaendelea na matibabu.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri amesema mashindano hayo yatasaidia sana kusisimua uchumi wa Jiji la Dodoma kwa kuwa majiji mengi yanachangamka kwa kuwa na shughuli mbalimbali kama hizo.
Pia amewashauri waandaaji wa mbio hizo kuwakumbuka watu wenye ulemavu na kuwaandalia mbio maalumu hali itakayosaidia kuamsha ali kwa watu wenye ulemavu kushiriki katika michezo kama ilivyo kwa tembo worious wanavyo wanavyoiwakilisha nchi.