Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI  NDEJEMBI AIELEKEZA TASAF KUJENGA UZIO SHULE YA SEKONDARI YA OLDONYOWAS ILI KULINDA MIUNDOMBINU YA SERIKALI

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Oldonyowas katika shule ya Sekondari Oldonyowas mkoani Arusha wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari Oldonyowas wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhandisi Richard Ruyango akimshukuru Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa shule ya Sekondari Oldonyowas Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bw. Anael Salakiki akisoma taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa TASAF katika Halmashauri hiyo.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu akisisitiza kutunza miundombinu ya majengo yanayojengwa katika Kijiji cha Oldonyowas Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri hiyo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akikagua nyaraka za ujenzi kwa ajili ya kujiridhisha na matumizi ya fedha zilizotolewa kwenye ujenzi wa bweni la wavulana shule ya Sekondari Oldonyowas wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Oldonyowas, Bi. Cecilia Sarakikya akitoa salamu za shukrani kwa TASAF kwa kuwezesha mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Oldonyowas mkoani Arusha wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

MUONEKANO wa bweni linalojengwa katika shule ya Sekondari Oldonyowas kwa ufadhili wa OPEC kupitia uratibu TASAF.

…………………………………………

Na. Veronica Mwafisi – Arusha

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameuelekeza uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kujenga uzio katika Shule ya Sekondari ya Oldonyowas iliyopo katika Kijiji cha Oldonyowas Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, ili kulinda miundombinu ya Serikali iliyojengwa kwa jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pamoja na kuimarisha usalama wa wanafunzi wa shule hiyo.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo, mara baada ya kukagua mabweni mawili ya wanafunzi wa kiume katika shule ya Sekondari Oldonyowas, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

“TASAF oneni ni kwa namna gani mtawezesha kwa haraka ujenzi wa uzio wa shule ya Sekondari ya Oldonyowas ili kuboresha usalama wa wanafunzi na kulinda miundombinu ambayo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametumia fedha nyingi za UVIKO katika kujenga mabweni ya wanafunzi wa kike na kiume pamoja na madarasa,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Kwa upande wake, mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Oldonyowas, Bi. Cecilia Sarakikya amesema ameupokea kwa mikono miwili mradi wa ujenzi wa mabweni kwasasabu utawasaidia watoto wao kupata sehemu ya kuishi katika mazingira ya shule, ikizingatiwa kuwa familia nyingi za wanafunzi wa shule hiyo ni za wafugaji ambao wanaishi pembezoni, hivyo kuwalazimu wanafunzi kutembea umbali mrefu ili kuhudhuria masomo.

Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu ameitaka kamati ya ujenzi kuhakikisha ujenzi wa mabweni unakamilika kwa kiwango kinachostahili.

Sanjari na hilo, Bw. Maduhu amewataka wananchi wa Kijiji cha Oldonyowas kuyatunza mabweni hayo pindi yatakapokamilika, ili yawe na manufaa katika kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu kwa watoto wa Kijiji hicho.

Mradi wa ujenzi wa mabweni mawili katika Kijiji cha Oldonyowas unaoendelea kukamilishwa, umefadhiliwa na OPEC kwa uratibu wa TASAF.

About the author

mzalendoeditor